Messi njoo huku, bosi wa Atletico amtaka kikosini

 MADRID HISPANIA. LIONEL Messi hana furaha kwa kile mabosi wa Barcelona walichomfanyia swahiba wake, Luis Suarez.

Mabosi hao wa Nou Camp wamemwondoa kihuni straika Suarez baada ya kocha mpya, Ronald Koeman kutua kwenye kikosi hicho na kumwambia fowadi huyo wa kimataifa wa Uruguay, hana chake tena kwenye timu hiyo, ruhusa kuondoka. Huku na huko, Suarez ametimkia zake Atletico Madrid alikonaswa na kocha Muargentina, Diego Simeone kwa ada ya Pauni 5.5 milioni jambo linalomfanya Messi kubaki mpweke huko Nou Camp kutokana na kumpoteza pacha wake wa ndani na nje ya uwanja.

Lakini, baada ya kusikia masikitiko ya Messi kuhusu Suarez, rais wa klabu ya Atletico Madrid, Enrique Cerezo amemwambia supastaa huyo wa Kiargentina anakaribishwa kwa mikono miwili aende Wanda Metropolitano kucheza pamoja na swahiba wake huyo, ambaye wamekuwa na urafiki wa karibu sana hadi kwenye familia zao.

Suarez ameondolewa Barcelona akiwa bado na mkataba wa mwaka mmoja na hawakuona shida kwa kumuuza kwa wapinzani wao kwenye La Liga.

Mechi yake ya kwanza tu, Suarez ameonyesha yeye ni balaa jingine ndani ya uwanja baada ya kufunga mara mbili na kuasisti mara moja katika dakika 19 tu alizochezea kwa mara ya kwanza timu yake mpya, Atletico ilipoichapa 6-1 Granada kwenye La Liga.

Kwenye kikosi cha Barcelona alikoondoshwa kama hana alichokifanya, staa Suarez alifunga mabao 198 katika mechi 283 alizocheza kwa misimu yake sita katika kikosi hicho huku Messi akikosoa sana kuondolewa kwa pacha wake kwenye safu ya ushambuliaji.

Messi mwenyewe alijaribu kufanya jaribio la kuondoka kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi, lakini Blaugrana waligoma kumwaachia bure, wakisisitiza anayetaka kumsajili basi aweke mezani Pauni 624 milioni kama kinavyobainishwa kipengele kilichowekwa kwenye mkataba wake.

Kwenye mchakato huo, Messi alidaiwa angekwenda mahakamani kulazimisha kuhama - lakini baadaye alikubali kubaki kwenye kikosi hicho kwa msimu mmoja zaidi huku akisema ameamua kuutikiza uongozi wa klabu kwa sababu anataka wafanye usajili wa maana.

Mkataba wa Messi utafika tamati Juni mwakani na Cerezo amefungua milango ya mkali huyo kwenda Wanda Metropolitano kukipiga sambamba na swahiba wake huyo.

“Kwenye maisha kama unataka kitu... Kama Leo Messi anataka kucheza na Luis Suarez, nataka nimwambie kitu kilekile, aje tu. Ukiwa na dhamira, kila kitu kinawezekana,” alisema.

Bosi huyo wa Atletico Madrid, Cerezo aliweka neno pia kuhusu rais wa Barcelona, Josep Maria Bartomeu akisema: “Kila kitu (kuhusu usajili Suarez) kilikwenda sawa. Bartomeu ni rafiki yangu na ni rais mzuri nina imani kila kitu kinakwenda sawa.

“Kwa wakati huu mambo yake hayaendi sawa Barcelona, lakini amekuwa akifanya kama hakuna kilichotokea. Suala la usajili wa Suarez halikusumbua kabisa, mchezaji amekwenda anakotaka kwenda kucheza.”