Meddie Kagere naitaka rekodi ya Mmachinga

Muktasari:

Naendelea kupambana kidogo kidogo katika kila mechi iliyokuwa mbele yangu naimani nitafikia malengo hayo kutokana na kiu ambayo ninayo lakini kwa jinsi ambayo nimejipima mwenyewe na timu yetu ilivyo naimani hilo linawezekana kama ligi tutafanikiwa kucheza tena.

POLENI na janga na corona. Ni matumaini yangu kwamba kila mmoja wetu anaendelea kujilinda vizuri pamoja na waliomzunguka. Tuombe Mungu azidi kutunusuru.

Kwa leo nitazungumzia rekodi za Ligi Kuu Bara. Hapa mchezaji ambaye anaongoza kufunga mabao mengi kwa miaka yote ni aliyekuwa mshambuliaji wa Yanga, Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ mwaka 1999, alipomaliza msimu akiwa amefunga mabao 26.

Katika kolamu yangu wiki hii nitaelezea hamu niliyonayo kuifikia rekodi hiyo ya ambayo imedumu kwa zaidi ya miaka 20, kutokana na malengo ambayo nimejiwekea na vitu ambavyo nimepanga kuvifanya msimu huu kama ligi itaendelea. Jambo la kwanza naangalia kila mechi iliyo mbele yetu kufunga bao ili kuongeza idadi kutoka kwenye yale niliyonayo, ingawa natambua sio jambo rahisi kufunga katika kila mchezo kutokana na ugumu wa wapinzani ambao tunakutana nao.

Ili niweze kufikia lengo la kufunga mabao 26, nimejiwekea lengo la kufikia kwanza mabao 23, ambayo nilifunga ligi msimu uliopita halafu ndio nitakuwa na chachu zaidi ya kuyavuka na kwenda kufikia rekodi nyingine kubwa kama hiyo ya Mmachinga.

Naendelea kupambana kidogo kidogo katika kila mechi iliyokuwa mbele yangu naimani nitafikia malengo hayo kutokana na kiu ambayo ninayo lakini kwa jinsi ambayo nimejipima mwenyewe na timu yetu ilivyo naimani hilo linawezekana kama ligi tutafanikiwa kucheza tena.

Mara nyingi huwa najiangalia mwenyewe kwanza kuzifikia rekodi zangu au kuzivunja na baada ya hapo ndio nawaangalia watu wengine waliokuwa mbele yangu jambo ambalo niliweza kuweka rekodi ya kufunga mabao 27, ndani ya msimu mmoja mwaka 2006. Mabao 27 nilifunga nikiwa nacheza Ligi Daraja la Kwanza Uganda katika timu ya PPU na kuweka rekodi ambayo haikufikiwa na mchezaji mwengine, lakini sijafahamu kama sasa kuna aliyeifikia au kuipita kwa kuwa sijawahi kuambiwa hilo. Kwa maana hiyo mabao 26 ambayo ni mengi zaidi kufungwa hapa nchini nina imani naweza kuyafikia.

Ukiachana na kuwa na kiu ya kufikia mabao mengi ambayo yalifungwa katika kolamu yangu ningependa pia kuelezea namna ambavyo kila ninapokwenda katika nchi kucheza soka huwa napewa majina tofauti kulingana na ambavyo nacheza soka.

Nikiwa nacheza ligi huko Uganda nilipewa jina la Six Cylinder, ambalo lilikuwa na maana ya kwamba nikiwa na mpira ni ngumu mpinzani wangu kuuchukua miguuni kwangu, lakini nilikuwa na uwezo mkubwa wa kukimbia jambo ambalo mashabiki wa soka walinibatiza jina hilo. Wakati huo nilikuwa nakimbia kwelikweli kama mwanariadha, na ilikuwa ngumu kama nikiwaacha mabeki wawili au watatu nyuma hata hatua moja kuweza kunifikia nikiwa na mpira au hata wakati sina.

Na jina hilo pia lilitokana na kuwepo magari ambayo yalikuwa na uwezo mkubwa wa kukimbia wakati huo kutokana na kuwekwa kifaa ambacho kiliitwa Six Cylinder.

Nikiwa nacheza Kenya nilipata majina mawili na kila moja likiwa na maana yake - jina la kwanza lilikuwa (Puff Man) na lingine Rwanda Magere na yote haya yalitokana pia na aina yangu ya kucheza uwanjani na majukumu ambayo nilikuwa nikiyatimiza.

Maana ya Puff Man ilikuwa ni mchezaji mwenye nguvu kushindana na mabeki wa timu pinzani na hata kama wakiwa na ubora kiasi gani kama nisipoweza kuwafunga, basi nitafanya madhara katika lango lao na ilikuwa hivyo, kweli nikabatizwa jina hilo.

Nikiwa naendelea kucheza Kenya nikapewa jina la Rwanda Magere ambalo awali sikujua maana yake na nilishangaa mashabiki walikuwa wakiniita tu nikiwa uwanjani, mtaani hata katika mitandao ya kijamii jambo ambalo lilinifanya kuwauliza wachezaji wenzangu.

Baada ya kuwauliza wachezaji wenzangu wa Gor Mahia pamoja na viongozi walinieleza kuwa maana ya jina hilo katika miaka ya nyuma nchini humu kulikuwa na shujaa wao aliitwa Rwanda Magere ambaye alikuwa haogopi vita na alikuwa mtu mwenye kupambana muda wote.

Huyo Rwanda Magere alikuwa akifanya mambo magumu na kuwashangaza wananchi wa Kenya - mambo ambayo yalishindwa kufanywa na watu wengi nchini humo. Sasa wakati nacheza na aina yangu ya kufunga mabao na kujitolea uwanjani ndio nikabatizwa jina hilo na mashabiki.

Nimekuja hapa Tanzania huu ni msimu wangu wa pili pia nimebatizwa majina mawili na mashabiki; MK 14, ambalo lina maana ya kwamba herufi mbili za kwanza katika majina yangu mawili pamoja na jezi namba ambayo navaa mgongoni.

Jina lingine ni Terminator ambalo limetokana na aina yangu ya kushangilia kwa kuziba jicho moja ambalo lilifananishwa na ‘muvi’ moja ya Ulaya ambayo ilichezwa na Arnold Schwarzenegger, ambaye naye alikuwa hana jicho moja lakini pia aina ya uchezaji wangu na ufiti nilionao, vyote vimechangia kubatizwa jina hilo.

Unajua Ijumaa ya wiki ijayo nitakuja na utamu gani? Kuna kitu nakiandaa kizuri sana. Usikubali kukikosa hapahapa kwenye Mwanaspoti. Lakini nakuomba tena na tena chukua tahadhari corona ni hatari, ila inazuilika ukiwa makini. Mimi sitoki ndani nimejifungia na familia yangu. Asanteni