Mechi zote 52 za Afcon laivu Azam UTV

Wednesday June 19 2019

 

Dar es Salaam. Kituo cha televisheni cha Azam UTV kitaonyesha mechi zote 52 za fainali ya Mataifa ya Afrika (Afcon) zitakazofanyika nchini Misri.

Mataifa 24 yanashiriki fainali hizo kwa mara ya kwanza ikiwa ni ongezeko la timu nane tofauti na fainali nyingine zilizokuwa zinashirikisha mataifa 16.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam Media, Tido Mhando amesema kituo chao cha Azam UTV kimepata haki ya kuonyesha mechi zote za mashindano hayo yanayoanza Juni 21 ambayo ni Ijumaa wiki hii.

Taifa Stars, ambayo inashiriki mashindano hayo kwa mara ya pili tangu mwaka 1980, imepangwa Kundi C pamoja na Algeria, Senegal na Kenya.

Tido, ambaye amewahi kuwa mkurugenzi wa Idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) amesema kutokana na fainali hizo, kituo chao cha Azam UTV kitabadilisha baadhi ya vipindi na taarifa ya habari ambayo imekuwa ikionyeshwa kuanzia saa 2:00 usiku mpaka saa 3:00 usiku sasa itakuwa ikionyeshwa saa 4:15 usiku mpaka saa 5:00 usiku.

Amesema watakuwa wakionyesha mechi zote tatu za kila siku za raundi ya mwanzo. “Mechi ya kwanza itakuwa saa 11:30 jioni, mechi ya pili saa 2:00 usiku na mechi ya tatu saa 5:00 usiku. Mechi zote hizi tutazionyesha moja kwa moja,” alisema.

Advertisement

Amesema hata matangazo ya Bunge ambayo wamekuwa wakiyaonyesha asubuhi mpaka jioni, sasa utaratibu wake utabadilika na watakuwa wakionyesha mpaka mchana kabla ya kuanza uchambuzi wa soka saa 10:00 jioni kila siku.

Tido amesema wakati wa mechi za robo fainali na nusu fainali, utaratibu wa taarifa ya habari unaweza kubadilika pia na itaanza kuonyeshwa saa 3:15 usiku mpaka saa 3:45 usiku kwa nusu saa tu.

Advertisement