Mechi tano kuamua tiketi fainali RBA

Wednesday September 30 2020

 

By Imani Makongoro

Dar es Salaam. Ushindi wa mechi tatu kati ya tano ndio utakaoamua timu zitakazofuzu kucheza fainali ya Ligi ya Mpira wa Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (RBA).

Katika mechi hizo, JKT itacheza na Oilers, ABC na Kurasini Heat katika hatua ya nusu fainali kwenye Uwanja wa Bandari - Kurasini, kuanzia kesho. Ili kufuzu kucheza fainali timu itapaswa kushinda mechi tatu mfululizo au mechi tatu kati ya tano.

“Kama timu ikishinda mechi tatu mfululizo itafuzu kucheza nusu, lakini zikipokezana kushinda zitarudiana hadi mechi tano ‘game five’ na itakayokuwa imeshinda 3-2 ndio itatinga fainali,” alisema jana mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BD), Okare Emesu.

Baadhi ya makocha na wachezaji wa timu hizo kila mmoja amekuwa akizungumzia ushindi na ubingwa, huku JKT ikitinga nusu fainali ikiwa na rekodi ya kutofungwa katika mechi 15 za ligi na mbili za robo fainali.

Nahodha wa JKT, Baraka Sadick alisema ndoto yao ni kuweka rekodi ya kutwaa ubingwa bila kufungwa, japokuwa wana mechi ngumu na Oilers, lakini wamejipanga kushinda.

Kocha wa ABC, Haleluya Kavalambi alisema licha ya kuifunga Kurasini Heat kwenye ligi wanapaswa kucheza kwa tahadhari. “Lazima tujipange, tumewasikia wanavyoapa kwamba hawapo tayari kufungwa tena na sisi, ila muda ndio utaamua, tuko vizuri, tuna ari na morali ya ushindi,” alisema Kavalambi.

Advertisement

Kocha Shendu Mwagalla wa Kurasini Heat alisema ndoto yao ni kucheza fainali, hivyo ni lazima waitimize.

 

Advertisement