Mdamu ana deni na Baraza

STRAIKA mpya wa Biashara United, Gerald Mdamu ameweka wazi kwamba msimu huu ana kibarua kizito cha kuonyesha kabisa kwamba kocha wake Francis Baraza hakufanya makosa ya kumsajili katika kikosi hiko.

Mdamu katika msimu uliopita alikuwa anaichezea Mwadui FC baada ya kumaliza mkataba katika kikosi hiko msimu huu amejiunga na Biashara Utd kwa mkataba wa mwaka mmoja.

Mshambuliaji huyo ameliambia Mwanaspoti kwamba anatakiwa kuhakikisha anafanya vizuri akiwa na kikosi hiko ili kocha wake aseme hakufanya kosa la kumsajili.

"Ukweli mwalimu ananiamini na ameona kabisa kwamba nina kitu na mimi nataka kumuaminsiha kwamba hakukosea kunisajili, njia pekee ni kufunga magoli nikiwa hapa."

Mdamu alisema licha ya kwamba anataka kufanya vizuri akiwa na kikosi hiko, amekumbana na changamoto ya mfumo mpya ambao ulianza kwa kumsumbua lakini sasahivi safi.

"Timu ni ngeni na nikakutana na mifumo tofauti na kule nilipotoka, hiyo ndio ilikuwa changamoto kubwa kwangu lakini nashukuru Mungu kwamba nimeshaanza kuelewa na kila kitu kitakuwa sawa."

Biashara mpaka sasa inashika nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi wakiwa na pointi 13 katika mechi sita.