Mchezaji anusurika kifo Morogoro, shabiki redcross aokoa maisha

Muktasari:

Hii si mara ya kwanza kwa wachezaji kupoteza fahamu kwenye Uwanja wa Sabasaba kwani katika ligi ya ndondo, nahodha wa timu ya soka ya Mangolo Fc, Abdallah Mtangwa Juni mosi mwaka huu alipoteza fahamu katika mchezo dhidi ya JL Dream Team.

Morogoro. Mfanyakazi wa Shirika la Msalaba Mwekundu ‘Red Cross’ mkoa wa Morogoro, Innocent Simon aliyekuwa jukwaani akitazama mechi kati ya Spider Fc na Mkundi United, ameibuka shujaa kwa kunusuru maisha ya mchezaji Ernest Zalalila aliyepoteza fahamu baada ya kugongwa katika mchezo wa ligi daraja la tatu mkoa wa Morogoro 2019/2020 uliofanyika kwenye Uwanja wa Sabasaba mkoani hapa.

Tukio hilo lilitokea katika dakika 85, wakati Zalalila wa Spider Fc alipogongana na kipa wa Mkundi United, Shauri na kupoteza fahamu uwanjani hapo hakukuwa na gari la wagonjwa wala watu wa huduma ya kwanza.

Kutokana na tukio hilo mwamuzi Fikiri Magari alilazimika kusimaisha mchezo kwa dakika tano ili kutoa nafasi ya kuokoa maisha ya mchezaji huyo.

Ndipo Simon mfanyakazi wa RedCross aliyekuwa amekaa jukwaani kutazama mchezo huo kama mashabiki wengine alipoona tukio hilo haraka aliingia uwanjani na kutoa huduma ya kwanza.

Akizungumza na Mwanaspoti uwanjani hapo, Innocent Simon alisema baada ya kuona mchezaji huyo amedondoka chini baada ya kugongana na kipa aligundua kuna shida amepata mchezaji huyo kwa namna alivyodondoka chini na mwamuzi aliposimamisha mchezo aliondoka jukwaani kukimbia kwenda uwanjani kumsaidia.

Innocent alisema kuwa wachezaji wenzake hawakuwa na mbinu za kumsaidia kurejesha fahamu.

“Yule mchezaji ujue amepoteza fahamu kwa zaidi ya dakika tatu na wachezaji wenzake hawakujua njia gani wanaweza kumsaidia zaidi ya kumwangalia tu, sasa kitu nilichofanya cha kwanza ni kuushika ulimi wake ambao ulikuwa unenda kwenye kolomeo na kurejesha kwenye hali yake ya awali na kumrejesha fahamu kwa kuchua mishipa ya nyuma ya shingo.”alisema Innocent.

Mchezaji huyo baada ya kurejea kwa fahamu zake alitolewa uwanjani hapo na kupelekwa hospitali kwa matibabu zaidi.

Kwa upande wa mwamuzi wa kati, Magari alisema alimruhusu mfanyakazi huyo wa Shirika la Msalaba Mwekundu (Red Cross), Innocent Simon kuingia uwanjani na kutoa huduma ya kwanza baada ya mabenchi ya ufundi ya timu hizo kukosa kuwa na madaktari wa timu.

Katika mchezo huo, Spiderv Fc ilifungwa mabao 2-1 na Mkundi United katika mchezo wa kutafuta timu zitakazofuzu kwa fainali bingwa wa mkoa wa Morogoro.

Mkundi United ilipata mabao yake kupitia, Shaqil Mohamed na Shabaan Mbewa huku bao la kufutia machozi la Spider lilifungwa na Aman Mganga.

Hii si mara ya kwanza kwa wachezaji kupoteza fahamu kwenye Uwanja wa Sabasaba kwani katika ligi ya ndondo, nahodha wa timu ya soka ya Mangolo Fc, Abdallah Mtangwa Juni mosi mwaka huu alipoteza fahamu katika mchezo dhidi ya JL Dream Team.