Mbona Djuma, Kichuya mambo freshi tu Simba

Thursday January 11 2018

 

LICHA ya winga machachari wa Simba, Shiza Kichuya kuonyesha utovu wa nidhamu wa hali ya juu kwa kumkasirikia kocha wake, Masudi Djuma baada ya kumtoa katika mechi dhidi ya URA na kununa karibu kupasuka, lakini kwa sasa mambo ni freshi tu.

Djuma alimtoa Kichuya katika dakika ya 45 wakati wakipoteza kwa bao 1-0 mbele ya Waganda na winga huyo kutoka kwa hasira huku akigoma kumpa mkono kocha wake, pia aligomea maji kutoka kwa daktari wa Simba, Yassin Gembe.

Pia Djuma aliwatoa tena Jonas Mkude, Mwinyi Kazimoto na Nicholas Gyan ambao nao walionyesha hali ambayo si ya kawaida kwani, waligoma kurudi kukaa benchi, lakini Djuma alisema; “Tulikuwa na presha ya kupata ushindi ndio maana kulitokea vitu kama hivyo, lakini hakuna la ziada.

“Tumeshazungumza na kuyamaliza hayo, sasa tunaendelea na majukumu yetu,” alisema Djuma ambaye mpaka sasa haifahamiki kama mabosi wake watamuidhinisha kuwa kocha mkuu kuchukua mikoba ya Kocha, Joseph Omog aliyetimuliwa klabuni hapo.

“Niwatoe hofu mashabiki na wapenzi wa Simba, wasiwe na wasiwasi, waungane kuipa timu nguvu katika mechi zote za ligi ili kuhakikisha tunafanya vizuri na kuchukua ubingwa,” aliongeza kocha huyo ambaye aliatua nchini kwa mbwembwe nyingi.