Mbelgiji abomoa ukuta Simba

Monday September 10 2018

 

By THOBIAS SEBASTIAN

ULE ukuta wa kikosi cha Simba ambao katika mechi mbili za Ligi Kuu Bara, haujaruhusu bao lolote unavunjwa. Ndio huu ni ukuta uliokuwa ukiundwa na mabeki visiki Pascal Wawa na Paul Bukaba akisaidiwa na mabeki wa pembeni, Asante Kwasi na Shomary Kapombe, wakimlinda kipa Aisha Manula.

Ukuta huo wa Simba chini ya Kocha Patrick Aussems kutoka Ubelgiji, umeruhusu jumla ya mabao 11 tu katika mechi 15 za mashindano zote ukiwamo wa juzi dhidi ya AFC Leopards ya Kenya. Mpango aliokuja nao Kocha Aussems ndio unaopelekea kwenda kuvunjwa na kuna mawili ama Pascal Wawa au Paul Bukaba utamfanya mmoja wao kuungana na Yusuf Mlipili kwenye benchi.

Katika mechi nyingi Kocha Aussems amekuwa akiwatupia Bukaba na Wawa kama mapacha wa beki ya kati na kuna wakati humtumia pia James Kotei, huku Mlipili aliyekuwa tegemeo msimu uliopita akiwa benchi kwa muda mrefu.

Kocha huyo ameifuatilia timu ya taifa, Taifa Stars ilipokuwa ikicheza mechi yake ya kuwania fainali za Afcon 2019 pale Kampala Uganda dhidi ya wenyeji wao, The Cranes na kushuhudia utamu wa beki Juuko Murshid.

Mbelgiji anasema alikuwa anasikia tu taarifa za Juuko, lakini hakuwahi kumfuatilia mpaka juzi alipomuona akifanya kazi kubwa wakati Uganda ikilazimishwa suluhu na Stars na kuagiza beki huyo arudi Msimbazi ili aje kuendelea na majukumu yake.

Aussems alisema kwa alivyomuona Juuko akiwazuia nyota wa Stars wasifanye mambo ameamini ataisaidia sana Simba kama atarejea kikosini kwani ni moja ya mabeki ambao anapenda awe nao kikosini.

Kama Juuko atarejea Msimbazi, basi lazima beki mmoja kati ya Wawa ama Bukaba atampisha Mganda huyo kuchukua nafasi moja na Kocha huyo alisema tangu alivyotua hapa nchini anafahamu kuwa Juuko ni mchezaji wa Simba, ila hajawahi kumuona tangu wakiwa kwenye maandalizi yao wakiwa Uturuki na hata waliporejea. Aussems alisema Juuko mpaka kasajiliwa na Simba kutoka nje ya nchi basi atakuwa ni beki mzuri, ila hafahamu kati yake na uongozi kuna shida gani mpaka kushindwa kuwa sehemu ya kikosi lakini natamani kuwa naye katika timu muda wowote.

“Kwa jinsi nilivyomuona kwenye mechi yao na Stars nimegundua ni mchezaji mzuri ambaye akiwepo katika timu ataongeza nguvu katika safu ya ulinzi,” alisema. “Beki mzuri wa kimataifa kweli anastahili na nitauomba uongozi kama itawezekana wamrudishe kikosini, lakini si vyema kuzungumza zaidi mchezaji ambaye hayupo kikosini, nipo tayari kuongeza nguvu zaidi ya hawa niliokuwa nao sasa,” alisema.

Kocha huyo alisema japo hakupata muda mrefu wa kulifuatilia pambano hilo kwa sababu ya maandalizi ya mchezo wao na Leopards, lakini aliona vitu vichache kwa Juuko na kukiri anafaa arudishwe Msimbazi.

“Alicheza vizuri kama alivyofanya Emmanuel Okwu, kwa muda niliowaona naamini Juuko ni mchezaji anayestahili kuendelea kuwepo hapa,” alisema Aussems.

KILA KITU FRESHI

Simba imecheza mechi mbili za Ligi Kuu kwenye uwanja wa nyumbani wa Taifa, jijini Dar na kuanzia wikiendi hii itasafiri kwa wiki mbili mfululizo mikoani, kitu ambacho Aussems amekiri sio tatizo.

Simba itaondoka jijini Alhamisi ili kwenda Mtwara kwa mchezo wao wa Jumamosi dhidi ya Ndanda wakiwa na rekodi ya kushinda mechi ya mwisho uwanjani hapo kwa mabao 2-0 na pia haijawahi kupoteza kabisa mjini humo.

Lakini ikitoka hapo itasafiri hadi Kanda ya Ziwa kuvaana na Mbao kisha Mwadui ambazo msimu uliopita waliibania kwa kutoka nao sare ya mabao 2-2 kila moja na kucheleweshwa mbio za ubingwa za Wana Msimbazi.

“Ratiba ndio imeshapangwa hatuna budi kukabiliana nayo lakini kwa jinsi ilivyo nitaendelea kuwaelekeza wachezaji wangu katika kila kile ambacho naona hakipo sawa kulingana na ratiba ili tuvune pointi tatu katika kila mechi,” alisema. “Nimepata muda wa kuona mechi ya Mbao na Mwadui msimu uliopita ambazo ziliisha kwa sare, lakini nina imani kubwa na timu yangu niliyokuwa nayo itakwenda kupata pointi zote sita katika mechi hizo mbili,” alisema Aussems.

“Kama benchi la ufundi tunaendelea kufanya kazi yetu na wachezaji watakwenda kufanya kazi yao ya kuhakikisha tunashinda mechi hizi.”

Advertisement