Mbelgiji: Mkude? Nyie acheni!

Friday April 3 2020

 

By Eliya Solomon


ALIYEKUWA Kocha wa Simba SC, Patrick Aussems amemtaja Jonas Mkude kuwa ni miongoni mwa wachezaji muhimu ambao waliifanya timu hiyo kufanya vizuri katika michezo ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2018/19.

Simba ikiwa chini ya kocha huyo raia wa Ubelgiji alifika hadi hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo waliondolewa kwa kufungwa jumla ya mabao 4-1 na miamba ya soka la DR Congo TP Mazembe.

Aussems ambaye alimtakia siku njema ya kuzaliwa Mkude siku mbili zilizopita, alimzungumzia kiungo huyo kwa kusema aliifanya Simba kuwa na nguvu katika eneo la kiungo kwa kushirikiana na James Kotei ambaye kwa sasa anacheza soka la kulipwa Belarus.

“Jonas ni mchezaji mzuri mwenye uwezo wa kuifanya timu kucheza kuanzia nyuma, alikuwa akifanya kazi kubwa na Kotei, nilikuwa nikiona tupo salama wakicheza pamoja, kuna muda yalikuwa yakitokea makosa ya kiuchezaji lakini ndio soka lilivyo,” alisema kocha huyo.

Aussems ambaye bado yuko kwao akisaka mchongo mpya, alifutwa kazi katika mazingira ya kutatanisha huku akiwa kipenzi cha mashabiki wa Simba.

Wakati akirejea kwao, Aussems alisema ili Simba ipige hatua inapaswa kuwa na viongozi makini ambao watakuwa na mitazamo mizuri na yenye tija kwa klabu hiyo.

Advertisement

Pamoja na kuwa Simba ilifanya vizuri msimu wa 2018/ 19 katika Ligi ya Mabingwa msimu uliofuata walijikuta wakiangukia pua kwa kushia hatua za awali kwa kuondewa na UD Songo ya Msumbiji, aliyokuwa akiichezea Luis Miquissone.

AONYA CORONA

“Tunapaswa kuwa wasimamiaji wazuri wa afya zetu hili linaenda kwa mtu mmoja mmoja. Corona ni hatari, hatupaswi kuuletea mzaha,” alisema.

Advertisement