Mbao FC haina kocha, yalia ukata

Muktasari:

Akizungumza na Mwanaspoti, Mwenyekiti wa klabu hiyo, Solly Njashi alisema ukata na ishu ya kumpata kocha ni mambo yanayowapa wakati mgumu kuanza mchakato wa usajili.

MWANZA.KLABU ya Mbao FC imeeleza sababu mbili za wao kuchelewa kufanya usajili kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu unaotarajia kuanza Agosti 23.

Dirisha la usajili linatarajia kufungwa mwishoni mwa mwezi huu na hadi sasa haijasajili mchezaji hata mmoja huku pia ikiwa haijulikani kocha gani atainoa.

Msimu uliopita timu hiyo ilinolewa na makocha watatu tofauti ikianza na Amri Said ‘Stam’, Ally Bushiri ‘Benitez’ na baadaye Salum Mayanga ambaye alitua mwishoni kukamilisha ligi.

Hata hivyo, timu hiyo tangu ipande Ligi Kuu msimu wa 2016/17 imekuwa ya kusubiri matokeo ya mechi ya mwisho kujinusuru kushuka daraja.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mwenyekiti wa klabu hiyo, Solly Njashi alisema ukata na ishu ya kumpata kocha ni mambo yanayowapa wakati mgumu kuanza mchakato wa usajili.

Alisema kwa sasa wanaumiza kichwa kuhakikisha wanakamilisha mpango wa kocha kisha wageukie usajili wa wachezaji jambo ambalo alidai wanalikamilisha

“Mayanga hatutakuwa naye kutokana na matatizo ya kifamilia aliyotueleza, tunapambana kumpata mbadala wake kisha kugeukia usajili wa wachezaji, lakini hali ya kiuchumi nayo inachangia,” alisema Njashi.