Mbao FC, Mbeya City kikaangoni

Muktasari:

Kule Mbarali, kwenye Uwanja wa Highland Estates Ihefu itaikaribisha Mbao FC ambayo ilimaliza nafasi ya 16 kwenye msimamo wa Ligi Kuu.

MICHEZO ya hatua ya mtoano kusaka timu mbili za kucheza Ligi Kuu msimu ujao zitachezwa kesho Jumatano kwa viwanja viwili kuwaka moto kati ya timu za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) na zile za Ligi Kuu.

Kule Mbarali, kwenye Uwanja wa Highland Estates Ihefu itaikaribisha Mbao FC ambayo ilimaliza nafasi ya 16 kwenye msimamo wa Ligi Kuu.

Ihefu baada ya kuisambaratisha Transit Camp wiki iliyopita hatua ya awali kwa mikwaju ya penalti 4-2 baada ya kutoa sare ya mabao 3-3 katika michezo yote miwili.

Geita Gold iliyotupa nje Majimaji kwa jumla ya mabao 4-2 nayo itakuwa nyumbani kukipiga na Mbeya City iliyomaliza nafasi ya 15 baada ya kuichapa bao  3-0 KMC mchezo wa mwisho wa ligi.

Wachimba Madini hao kutoka Geita ni msimu wao wa pili sasa inafika hadi hatua hiyo, msimu uliopita ilitupwa nje na Mwadui FC na sasa inatupa upya karata yake.

Ihefu ilimaliza nafasi ya pili Kundi A ikiwa na alama 51 sawa na Dodoama Jiji FC iliyokuwa na idadi nzuri ya uwiano wa mabao na kupata nafasi ya kupanda moja kwa moja kucheza Ligi Kuu msimu ujao.

Geita Gold FC kwa upande wao ilimaliza nafasi ya pili Kundi B ikiwa na alama 34 huku Gwambina FC ikiwa kileleni kwa alama 47.

Kocha wa Ihefu, Maka Mwalwisa amesema wanaelekea kwenye hatua ngumu zaidi ya walikotoka sababu wanakutana na timu iliyokuwa ligi daraja la juu.

"Kila mmoja ana matumaini ya kucheza Ligi Kuu, hii ni fursa kwetu sina neno la kuwaambia wachezaji wangu na mashabiki zaidi ya kuwaomba kila mmoja ajitoe kwa nguvu zote.

"Tumepambana, safari ilikuwa ndefu na ngumu, sasa ndio muda wa kuhakikisha tunatekeleza lengo letu la kucheza Ligi Kuu msimu ujao," amesema Mwalwisa.

Kocha wa Mbao FC, Fredy Felix 'Minziro' amesema kila kitu kinawezekana japo wanakutana na timu ambayo hawajawahi hata kuiona ikicheza.

Minziro ametua Mbao FC, kazi yake kubwa ni kuinusuru timu hiyo isishuke daraja. Wakati akipewa jukumu hilo Mbao ilikuwa imecheza mechi 30, na alama zao 25 ikishika nafasi ya 19.

Imecheza michezo nane bila kupoteza, akishinda michezo sita na sare mbili, akitoa suluhu mbele ya Prisons na baadaye kutoka sare ya bao 1-1 na JKT Tanzania.