Mbao, Mbeya City mbona kazi wanayo

Muktasari:
Mbao wanahitaji ushindi kuanzia mabao 3-0 dhidi ya Ihefu ili kubaki Ligi Kuu, huku Mbeya City wao wakihitaji suluhu au ushindi wowote ili kuwaondosha wapinzani wao Geita Gold ya Daraja la Kwanza.
WAKATI mchezo wa marudio kati ya Mbao na Ihefu wa kusaka timu ya kupanda au kubaki Ligi Kuu ukitarajia kupigwa leo jioni katika dimba la CCM Kirumba jijini hapa, wenyeji Mbao wanahitaji ushindi wa mabao kuanzia 3-0 ili kujihakikishia kuendelea kuziona Simba na Yanga.
Mchezo huo wa mtoano 'Play Off' unatarajia kuwa mgumu haswa kwa Mbao, kwani mechi ya awali wakiwa ugenini jijini Mbeya walikubali kulala kwa mabao 2-0 hivyo kuwafanya leo kucheza kufa na kupona kupata matokeo mazuri.
Kazi nzito itakuwa itakuwa kwa mabeki wao wakiongozwa na nahodha wao, Babilas Chitembe ambao watakuwa na shughuli ya kuwazuia washambuliaji wa timu pinzani kutoruhusu lango lao kuguswa huku Kipa naye, Rahim Sheikh akipaswa kuwa imara kutokana na kuaminiwa na benchi la ufundi.
Hata safu yao ya ushambuliaji ikiongozwa na kinara wa mabao kikosini humo, Wazir Junior watakuwa na kibarua kigumu katika kutumia vyema nafasi watakazopata ili kuinusuru timu yao kutoshuka Daraja kwani Mbao ndio imebaki baada ya majirani zao, Alliance FC kushuka mapema katika zile timu nne.
Wakati huohuo hekaheka nyingine itakuwa jijini Mbeya pale Mbeya City itakapowakaribisha wapinzani wao, Geita Gold katika mechi ya mwisho ya kujua hatma kwa timu hizo kujua nani anaungana na miamba ya soka nchini, Simba na Yanga.
Hata hivyo Mbeya City wanashuka dimbani wakiwa na hesabu nzuri kutokana na mechi ya awali kutoa sare ya bao 1-1 hivyo iwapo watamaliza dakika 90 za leo kwa suluhu au ushindi wowote watajihakikishia kubaki Ligi Kuu msimu ujao.
Kazi kubwa leo itakuwa kwa Geita Gold ambao watahitaji kupata ushindi au sare ya kufungana mabao ili kufanya mechi hiyo kuamuriwa kwa mikwaju ya penalti na mshindi kupanda Daraja.