Matola njia nyeupe Simba SC, Polisi Tanzania yampa mkono wa kwa kheri

Muktasari:

Tangu kutimuliwa kwa kocha Patrick Aussems ndani ya Simba jina la Matola limekuwa likitajwa kwenda kuchukua mikoba hiyo

Moshi. Uongozi wa klabu ya Polisi Tanzania umethibitisha kuachana na kocha wake Msaidizi Selemani Matola aliyepata ajira katika timu nyingine.

Uamuzi huo wa Polisi kuachana na Matola unathibisha taarifa kwamba kocha huyo sasa yupo mbioni kutua Simba kuchukua jukumu la Denis Kitambi.

Akizungumzia suala hilo, kaimu katibu mkuu wa Polisi Tanzania, Frank Geoffrey amesema baada ya kupokea na kukubaliana na ombi la Matola juu ya kuvunja mkataba.

"Kwa sasa bado tunashughulika na ombi lake la kuvunja mkataba maana lina hatua kadhaa za kuzifuata na tukimaliza hilo naamini tutaanza kujadili majina yaliyopendekezwa mezani juu ya nani awe kocha msaidizi."

Alisema kuwa jukumu la kupendekeza majina ya wasaidizi wake wamelitoa kwa kocha wao mkuu Ally Mtuli hivyo wanaamini watakapomaliza mikakati ya kuvunja mkataba watakaa kikao kuyajadili na kuyaweka wazi mezani.

"Katika kikao cha viongozi na  kamati ya ufundi tuliyokaa hivi karibuni na kuridhia kuvunja mkataba, tulitoa nafasi kwa mkurugenzi wa benchi la ufundi ambae ndio Kocha Mtuli aanze kusambaza macho yake kutafuta msaidizi wake hivyo akipendekeza hata kocha Mbwana Makata arudi sisi tutamkubalia tu maana ndio pendekezo lake" alisema Frank.