Matatizo ya kiafya yampa sonona Pele

Muktasari:

Sonona kwa lugha ya kitabibu ni depression ni tatizo ambalo linaweza kumpata mwanadamu pale anapokumbwa na jambo kubwa la kuumiza hisia zake.

GWIJI wa soka duniani ambaye anatajwa kama mwanamichezo bora wa karne ya 21 duniani, Pele amepatwa na tatizo la kiakili la sonona kiasi cha kumfanya kutopenda kujitokeza hadharani.

Pele ambaye jina lake halisi ni Edson Arantes do Nascimento ambaye mwaka huu anatimiza miaka 80 amekuwa na matatizo makubwa ya kiafya ikiwamo la karibuni la nyonga na ya zamani mgongo, goti na figo.

Tatizo la sonona lilijitokeza zaidi mara baada ya kufanyiwa upasuaji wa nyonga mwishoni mwa mwaka uliopita hali inayosababisha kuhitaji usaidizi kwa kutembelea kiti cha matairi.

Hali aliyonayo sasa iliwekwa bayana na mtoto wake wa kiume ajulikanye kama Edinho mwenye umri wa miaka 49 anasema baba yao amekuwa mkali asiye na furaha na hapendi kutoka hadharani kabisa.

Mwanaye alieleza hayo siku ya Jumatatu katika televisheni ya Globoespote ya nchini Brazili kuwa baba yake tangu ashindwe kutembea vyema amekuwa anajitenga akiona aibu kutoka.

Sonona kwa lugha ya kitabibu ni depression ni tatizo ambalo linaweza kumpata mwanadamu pale anapokumbwa na jambo kubwa la kuumiza hisia zake.

Ni dhahiri kuwa upasuaji ya nyonga na kuwekewa nyonga ya bandia na kutoweza kutembea kwa kujitegemea kunamfanya kupata hali hiyo ya huzuni kali.

Pele tangu alipostaafu soka tayari ameshafanyiwa upasuaji zaidi ya mara 7 na huku akilazwa mara kwa mara kutokana na nimonia na uambukizi njia ya mkojo.

Mtakumbuka pia tangu mwaka 1970 anaishi na figo moja tu hii ni baada ya kudondoka katika mechi na kuvunja mbavu ambayo ilijeruhi figo yake hivyo madaktari kulazimika kuiondoa kwa upasuaji.

Upasuaji wa pili na wa tatu ambao ni wa mfupa wa paja na tezi dume mwaka 2012 miezi tofauti na wa nne ni ule wa uti wa mgongo uliofanyika Julai 2015 baada ya pingiri kuhama na kubana mishipa ya fahamu.

Upasuaji wa tano ni kuondoa vijiwe katika figo ulifanyika Novemba 2015 na kurudiwa tena mwaka jana mwezi wa nne baada ya kupata shambulizi la njia ya mkojo.

Upasuaji wa saba ndiyo wa nyonga uliofanyika karibuni ambao kwa kiasi kikubwa umemweka mfalme huyo wa soka katika hali ya kushindwa kutembea kwa kujitegemea.

Mwanae alieleza zaidi kuwa baba yake amepatwa na hali ya kushindwa kutembea hasa baada ya programu ya uponaji ya mazoezi tiba ili kurudishaji utendaji wa nyonga kutofanyika vizuri.

Kuandamwa huku kwa magonjwa haya na umri mkubwa alionao ni vitu ambavyo vimedhorotesha afya yake na kumnyima furaha nguli huyo wa soka ambaye enzi zake ametwaa ubingwa wa dunia mara tatu.

Itakumbukwa pia mwaka jana mwezi wa nne alipata mwaliko maalum jijini Paris, Ufaransa kuhudhuria hafla ya kampeni akiwa na pamoja na mshambuliaji wa PSG Kylian Mbappe.

Mara tu hafla hiyo kumalizika alianza kujisikia ovyo na kukimbizwa hospitali jijini Ufaransa na baadaye siku tano alirudishwa Brazili kufanyiwa upasuaji katika hospitali ya Albert Einstein kuondoa vijiwe katika figo.

Kabla ya tatizo la nyonga matatizo ya muda mrefu ya uambukizi njia ya mkojo, shambulizi la tezi dume, mgongo na nimonia ni vitu ambavyo kwa miaka ya karibuni vimekuwa vikimpata mara kadhaa na kulazwa.

Mambo haya yote yalikuwa yanaashiria kuwa afya yake si njema kuweza kuhimili mikimikimiki ya kujumuika na matukio mbalimbali ya kijamii ikiwamo matamasha na mashindano.

Matatizo yote haya ya kiafya ni kama vile yamechangia kumpa huzuni kali hatimaye kupata sonona.

Kitabibu huwa ni jambo la kawaida kwa mgonjwa yeyote anayeugua kupata sonona au huzuni kali ambayo ni tatizo la kuathirika kwa afya ya akili hali ambayo isipodhibitiwa huleta madhara makubwa ya kiakili.

Kuwa maarufu kama mfalme wa soka duniani ambaye amefunga magoli kwa rekodi bora ya 1, 281 katika mechi 1,363 ndani ya miaka 21 ya kucheza soka kunamfanya kuumia sana kihisia.

Ucheshi wake akiwa kama balozi katika mambo mbalimbali ya soka kunamfanya sasa ajione hana thamani na kuona aibu kujitokeza hadharani akiwa na usaidizi wa kitu maalum au magongo.

Je nini kifanyike

kukabiliana na

sonona?

Sonona inaweza kutibiwa kwa dawa na tiba ya ushauri nasaha na wataalam wa afya ya akili ambao hutumia utabibu wa kiakili kwa kufanya urekebishaji tabia kwa kubadili fikra hasi na tabia zinazoleta huzuni.

Pele atahitajika kusaidiwa na wataalam wa afya ya akili na pengine kwa hadhi yake litakuwa limeanza kufanyiwa kazi.

Mwenye tatizo hili anahitaji sana faraja.