Mastaa wa Ufaransa waliokipiga Barcelona

Muktasari:

Lakini katika zama za hivi karibuni kumekuwa na mastaa ambao kizazi cha sasa kinaweza kuwakumbuka zaidi.

BARCELONA,HISPANIA.BARCELONA imefanikiwa kuinasa saini ya winga mahiri wa kimataifa wa Ufaransa, Antoine Griezmann kutoka Atletico Madrid.

Huyu si Mfaransa wa kwanza kukipiga Nou Camp. Zamani kulikuwa na mastaa wa Kifaransa waliocheza Nou Camp kama kina René Victor Fenouillère (1902-1903), Henry Normand (1908-1909), Jim Carlier (1913-1914), Maurice Bigué (1913-1914), Jean Verdoux (1917-1918), Peijean (1928), Jules Robisco (1948) na Lucien Müller (1965-1968).

Lakini katika zama za hivi karibuni kumekuwa na mastaa ambao kizazi cha sasa kinaweza kuwakumbuka zaidi.

Laurent Blanc (1996-1997)

Staa wa zamani wa kimataifa wa Ufaransa ambaye alijulikana kwa utulivu wake uwanjani. Blanc alijiunga na wababe hawa wa Nou Camp mwaka 1996 akitokea kwao Ufaransa katika Klabu ya Auxerre.

Akiwa na Barcelona alionyesha ubora wake lakini muda mwingi alijikuta akiwa majeruhi. Alidumu klabuni hapo kwa mwaka mmoja tu kabla ya kutimkia Italia.

Christophe  Dugarry (1997-1998)

Staa mwingine wa kimataifa wa Ufaransa ambaye aliichezea Barcelona kwa msimu mmoja tu. Alijiunga nayo akitokea AC Milan ya Italia na kutwaa ubingwa wa La Liga katika msimu wake huo huo wa kwanza na wa mwisho. Ingawa anahesabika alitwaa Kombe la Dunia na Ufaransa akiwa mchezaji wa Barcelona lakini mara baada ya michuano hiyo alirudi nyumbani kwao Ufaransa kujiunga na Lyon.

Frèderic Déhu (1999-2000)

Hatujui kulikuwa na ugonjwa gani uliokuwa unawaandama mastaa wa Ufaransa katika dimba la Nou Camp wakati huo. Huyu ni staa mwingine wa Ufaransa ambaye alidumu klabuni hapo kwa msimu mmoja tu. Alijiunga na wababe hao wa Catalunya akiwa ametoka kuchukua ubingwa wa Ufaransa na Klabu ya RC Lens. Alicheza kwa msimu mmoja Nou Camp kabla ya kurudi kwao Ufaransa akisaini PSG.

Emmanuel Petit (2000–2001)

Kiungo mahiri wa kimataifa wa Ufaransa ambaye alitwaa Kombe la Dunia na Ufaransa mwaka 1998 kama ilivyo kwa Duggary.

Petit alitamba mno katika safu ya kiungo cha Arsenal akiwa sambamba na Mfaransa mwenzake, Patrick Vieira lakini mwaka 2000 aliamua kuachana na klabu hiyo iliyokuwa na makazi yake Highbury na kwenda kujaribu bahati yake Barcelona. Hata hivyo, aliishia kuchezeshwa kama beki wa kati na wakati mwingine kama beki wa kushoto. Na yeye aliingia katika mkumbo wa wachezaji wa Kifaransa waliodumu msimu mmoja tu klabuni hapo. Baada ya msimu huo alirudi England kujiunga na Chelsea.

Philippe Christanval (2001-2003)

Beki wa kimataifa wa Ufaransa ambaye walau aliweza kudumu kwa misimu miwili klabuni hapo. Alijiunga na Barcelona akitokea AS Monaco ya Ufaransa lakini licha ya kudumu kwa misimu miwili Nou Camp alijikuta akicheza mechi 32 tu kabla ya kurudi tena nyumbani na kusaini Marseille.

Ludovic Giuly (2004-2007)

Staa mwingine wa kimataifa wa Ufaransa ambaye alitua Nou Camp akitokea Monaco ya Ufaransa. Giuly anabakia kuwa mmoja kati ya wachezaji wa Kifaransa wenye mafanikio makubwa Barcelona. Alikuwa sehemu ya kikosi cha Kocha, Frank Rijkaard ambacho kilitwaa ubingwa wa Ulaya kwa kuichapa Arsenal katika pambano la fainali Stade de France Mei 2006. Mwaka mmoja uliofuata alibadilisha upepo kwa kwenda kucheza soka Italia katika Klabu ya AS Roma.

Ludovic Sylvestre (2005-2006)

Ludovic ni Mfaransa mwingine ambaye aliwahi kucheza Barcelona akitokea Ufaransa. Huyu alinunuliwa kutoka katika Klabu ya Kayseripor ya Uturuki kwa ajili ya kuchezea Barcelona B.

Hata hivyo, aliwahi kuambulia kucheza mechi mbili za Barcelona ya wakubwa katika La Liga. Baada ya hapo aliona maji ni mazito na akaamua kutimkia Sparta Prague ya Czech.

Lilian Thuram (2006-2008)

Mmoja kati ya mabeki bora kuwahi kutokea katika soka la Ufaransa. Kama ilivyo kwa Duggary na Petit alikuwemo katika kikosi cha Ufaransa kilichotwaa Kombe la Dunia Ufaransa mwaka 1998.

Aliwasili klabuni hapo mwaka 2006 baada ya kucheza soka Italia kwa muda mrefu. Alitua akitokea Juventus na kuichezea Barcelona kwa misimu miwili. Thuram alitwaa Super Cup, Hispania mwaka 2006 akiwa na Barcelona.

Thierry Henry (2007-2010)

Anabakia kuwa mchezaji bora wa muda wote Arsenal. Baada ya kutamba Highbury kisha Emirates na kuandika historia ya kuwa mfungaji bora wa muda wote Arsenal, hatimaye staa huyu wa kimataifa wa Ufaransa ambaye pia alitwaa Kombe la Dunia na Ufaransa mwaka 1998, aliamua kuondoka klabuni hapo mwaka 2007 na kwenda Barcelona kujaribu kutengeneza historia mpya. Akiwa na Barcelona alitwaa mataji kadhaa ikiwemo taji la ubingwa wa Ulaya mwaka 2009.

Éric Abidal(2007-2013)

Kando ya Giuly, huyu naye anabakia kuwa Mfaransa mwenye mafanikio zaidi katika historia ya Barcelona. Aliichezea klabu hii ya Catalunya kwa miaka sita na kutwaa karibu kila kitu chini ya kocha mtaalamu, Pep Guardiola.

Abidal pia aligeuka shujaa miongoni mwa watu wa Catalunya nje ya uwanja baada ya kufanikiwa kuushinda ugonjwa wa kansa mara mbili.

Aliondoka mwaka 2013 kwenda kujiunga na Monaco ya kwao Ufaransa lakini kwa sasa amerudi tena klabuni hapo akiwa mmoja kati ya wakurugenzi wa klabu hiyo.

Jéremy Mathieu (2014-2017)

Beki mrefu wa kimataifa wa Ufaransa ambaye alitua Nou Camp mwaka 2014 akitokea kwa wababe wengine wa Hispania Valencia.

Hata hivyo, Mathieu ambaye alikuwa na uwezo wa kucheza kama beki wa kati na beki wa pembeni baada ya misimu mitatu Nou Camp aliruhusiwa kwenda Sporting Lisbon ya Ureno.

Samuel Umtiti (2016)

Beki mwingine wa Kifaransa ambaye alitwaa Kombe la Dunia na Ufaransa lakini katika kizazi kingine. Umtiti alinunuliwa na Barcelona mwaka 2016 akitokea Lyon na mpaka sasa amekuwa akikipiga klabuni hapo ingawa mara kadhaa jina lake linatajwa katika orodha ya wachezaji ambao wanaweza kuondoka.

Lucas Digne(2016-2018)

Beki wa kushoto wa kimataifa wa Ufaransa. Digne alijiunga na Barcelona akitokea PSG katika dirisha kubwa la majira ya joto mwaka 2016. Mambo hayakwenda sawa kama ilivyotegemewa na katika dirisha kubwa la mwaka jana Barcelona ilimuuza kwenda Everton ambako amegeuka kuwa tegemeo.

Ousmane Dembele (2017-)

Nyota wa kimataifa wa Ufaransa ambaye Barcelona ilimnunua kwa dau kubwa la Pauni 146 milioni kwa ajili ya kuziba nafasi ya staa wa Brazil, Neymar aliyeuzwa kwenda PSG. Dembele amekuwa akisumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara na pia amekuwa akihusishwa kuondoka klabuni hapo.

Kununuliwa kwa Griezmann kunamuweka pamoja na staa mwenzake huyu wa kimataifa wa Ufaransa lakini ni wazi kunafungua mchuano mkali wa namba baina yao.