Mastaa Yanga wataja sifa za kocha mpya

Muktasari:

Jana Jumatatu, Yanga ilitangaza kumtimua kocha wao Eymael kutokana na sauti iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii ikionyesha ubaguzi kwa mashabiki na kauli zisizo za kiungwana na kiuanamichezo zilizotolewa na kocha huyo.

NAHODHA Msaidizi wa Yanga, Juma Abdul amesema kuondoka kwa kocha Luc Eymael kumewaumiza kama wachezaji, lakini ameomba uongozi kutafuta kocha mwenye viwango vya kimataifa pamoja na kusajili wachezaji wa maana ili kuendana na muda uliopo

Jana Jumatatu, Yanga ilitangaza kumtimua kocha wao Eymael kutokana na sauti iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii ikionyesha ubaguzi kwa mashabiki na kauli zisizo za kiungwana na kiuanamichezo zilizotolewa na kocha huyo.

Kocha huyo ametimuliwa wakati Ligi Kuu Bara ikiwa imemalizika huku wachezaji wa Yanga wakipewa wiki mbili tu za mapumziko kabla ya kurejea mazoezini.

Abdul ameliambia Mwanaspoti jijini Dar es Salaam leo Jumanne, Julai 28, 2020 kuwa anaamini kutokana na muda mchache uliopo itakuwa ngumu kwa wao kuelewana haraka na kocha mpya hivyo uongozi wanapaswa kumleta kocha mwenye kiwango cha juu sana ambaye hatakuwa na mambo mengi.

"Tumesikitika kuondoka kwa Eymael kwani kama wachezaji tuliishi naye vizuri na kama unavyojua hata katika familia mkizoeana mmoja anapoondoka inakuwa ni huzuni.

"Hata hivyo maisha lazima yaendelee na naamini uongozi uko kwenye mchakato wa kumtafuta kocha mpya maana ukiangalia muda ni mdogo kabla ya kuanza msimu mwingine wa ligi.

"Kazi itakuwepo kwani hakuna kitu kigumu kama kubadilishiwa kocha halafu ni muda mfupi kabla ya ligi, inakuwa ngumu kuelewana haraka nikimaanisha kushika falsafa zake. Ndio maana timu inatakiwa kuwa na kocha karibu mwaka mzima ndio inakuwa sawa na kucheza kwa ubora wake", amesema Abdul.

Ameongeza; "Nimesikia Yanga inakwenda kufanyiwa marekebisho ikiwa na maana wachezaji wengi wataondoka. Sasa ikiwa wengi wataondoka ina maana watakuja wengi wapya ambao wataungana na wale wachache watakaobaki kikosini halafu wanakutana na kocha mpya, hapo ugumu sasa ndio utakapokuwepo.

"Muhimu ninachowaomba viongozi, watafute kocha mwenye kiwango kikubwa ambaye  tutamuelewa kwa muda mfupi na pia wasajili wachezaji wenye viwango ili timu isiyumbe kama ilivyokuwa msimu uliopita.

"Naamini kama uongozi utafanya, ikiwemo kuongeza wachezaji wenye ubora watakaoshirikiana na wale watakaobaki basi msimu ujao  unaweza kuwa mzuri kwetu," amesema Abdul.