Mashine sita kurudisha heshima ya Man United

Muktasari:

Baada ya kufanya usajili wa kiungo Bruno Fernandes kwenye dirisha la Januari, Woodward ametoa orodha ya mastaa sita ambao atasimamia dili zao za kujiunga na timu yake katika dirisha la kiangazi huko Ulaya.

MANCHESTER, ENGLAND . MANCHESTER United wameripotiwa kutenga mkwanja wa Pauni 160 milioni ili kuwanasa mastaa wawili wa Kingereza, Jack Grealish na James Maddison.

Hata hivyo, unaambiwa hiyo ni sehemu chache tu ya mastaa ambao bosi kubwa wa Man United, Ed Woodward amepanga kuwashusha ndani ya wababe hao wa Old Trafford.

Baada ya kufanya usajili wa kiungo Bruno Fernandes kwenye dirisha la Januari, Woodward ametoa orodha ya mastaa sita ambao atasimamia dili zao za kujiunga na timu yake katika dirisha la kiangazi huko Ulaya.

“Mpango wetu wa usajili unatazama na kujadili aina ya wachezaji tunaowataka katika dirisha lijalo,” alisema Woodward, ambaye ni makamu mwenyekiti mtendaji wa klabu hiyo.

“Ikiwa ni sehemu ya kujiimarisha na kujenga timu, tunaona nafasi nzuri ya kufanya usajili kwenye dirisha lijalo. Usajili wa Bruno na kurejea kwa wachezaji wetu muhimu waliokuwa majeruhi kutampa nguvu Ole kumalizia nusu iliyobaki ya msimu.

“Bado tunachuana kwenye Europa League na Kombe la FA. Tunachuana pia kuwania nafasi ya kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini bodi inatazama jinsi ya kufanya mambo kuirudisha timu kwenye ushindani wa Ligi Kuu England na Ligi ya Mabingwa Ulaya.”

Taarifa zaidi zinadai kwenye orodha hiyo ya wachezaji sita, si pungufu ya wachezaji watatu watanaswa kwenda kukipiga Man United wakati wa dirisha la usajili wa majira ya kiangazi litakapofunguliwa.

Mastaa hao sita ni Grealish, Maddison, Donny van de Beek, Jadon Sancho, Jude Bellingham na Kalidou Koulibaly.

Katika kupata pesa za kuwanasa mastaa wote hao, Man United inafungua milango ya wachezaji wengine kuondoka, akiwamo Paul Pogba ambaye inaamini itapiga pesa ndefu kwenye kumuuza na kuokoa pia mkwanja mrefu kwenye malipo ya mishahara inayomlipa kila wiki. Hata hivyo, Man United imekuwa ikihusishwa sana na mastaa mbalimbali wakali wakati wa usajili, lakini mwisho wa siku hushindwa kukamilisha dili hizo.