Mashemeji Derby: Mechi ya Heshima, machozi, jasho na damu

Muktasari:

Mahesabu yanathibitisha kwamba, Ingwe ni wababe wa vita kama hivi, wamekutana zaidi ya mara 83, mechi ya leo ikiwa ni ya 84, AFC Leopards wakiongoza kwa kushinda mechi nyingi ambapo takwimu zinasema wameshinda mara 27, Gor Mahia wakishinda mara 25, matokeo ya sare yakiwa ni 31.

Nairobi, Kenya. Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Kenya, Gor Mahia wanahitaji pointi moja tu ili kutetea taji hilo kwa mara ya 17.

Gor Mahia wanaongoza msimamo wakiwa na pointi 68, baada ya kushuka uwanjani mara 27, ambapo tofauti ya pointi kati yao na Bandari inayoshika nafasi ya pili ni pointi 20.

Kwa mujibu wa ratiba ya KPL, leo Jumamosi Agosti 25, 2018 wanakutana na mahasimu wao wakubwa katika historia ya soka la Kenya, AFC Leopards, katika mechi ya kukata na shoka ya mashemeji derby, itakayopigwa ugani Kasarani kuanzia saa 10 jioni na kushuhudiwa na mashabiki wapatao 60,000. Patachimbika!

Itakuwa ni mechi ya kisasi, jasho, machozi na damu. Baada ya kukutana mara tatu msimu huu, Kogalo wakiibuka wababe, ni lazima wataingia Kasarani wakiwa na mpango wa siri. Lazima vijana wa Muargentina Rodolfo Zapata, watataka kumzuia Muingereza Dylan Kerr na wahuni wenzake wa jeshi la kijani.

Rekodi haidanganyi. Mahesabu yanathibitisha kwamba, Ingwe ni wababe wa vita kama hivi, wamekutana zaidi ya mara 83, mechi ya leo ikiwa ni ya 84, AFC Leopards wakiongoza kwa kushinda mechi nyingi ambapo takwimu zinasema wameshinda mara 27, Gor Mahia wakishinda mara 25, matokeo ya sare yakiwa ni 31. Namba hazidanganyi.

Tangu mwaka 1968, ilipopigwa mechi ya kwanza ya mashemeji derby, bao la kwanza likiwekwa kambani na Mkongwe Joe Kadenge, tayari mabao 149 yameshawekwa kimiani, (AFC Leopards 75, Gor Mahia 74), bao la 149 likifungwa na kiungo mshambuliaji wa Gor Mahia George 'Blackberry' Odhiambo. Nani atafunga bao la 150?

Kabla ya kuelekea Kasarani kitu kingine ambacho msomaji wa Mwanaspoti unapaswa kufahamu ni kwamba, zaidi ya mechi 14 zilizokutanisha miamba hii miwili, zote zilimalizika kwa ushindi wa 2-1, ukiwemo mchezo wa kwanza (1968), ambao Kogalo waliibuka kidedea.

Mbali na matokeo hayo ya 2-1, ni mechi 24 za mashemji derby, ziliisha kwa ushindi mwembamba wa 1-0, huku 18 zikienda sare, swali kubwa ni je, matokeo ya leo yatakuwaje? itakuwa 2-1, 1-0, 0-0 au kutakuwa na kapu la mabao? tusiandikie mate!

Kuelekea Kasarani, rekodi pia zinaonesha kuwa, tukiachana na habari za Joe Kadenge na William 'Chege' Ouma waliotupia kwenye mtanange wa kwanza pale Nairobi City Stadium, ni kwamba wachezaji watatu tu ndio waliojifunga wenyewe kwenye mechi za mashemeji derby.

Wachezaji hao, ni nahodha wa zamani wa Musa Mohammed aliyejifunga katika sare ya 1-1, Agosti 27, 2017. wengine ni Allan Huma wa AFC Leopards (mwaka 2009) na Hamisi Shamba wa Gor Mahia (mwaka 1981).

 

MEDDIE KAGERE KINARA WA MABAO

Achana na habari ya mabao mawili aliyofunga Chege mwaka 1968, Straika wa sasa wa Simba ya Tanzania, Mnyarwanda Meddie Kagere, ndiye Baba yao.

Nyota huyu aliyeitumikia Kogalo kwa misimu mitatu ya mafanikio, anaongoza kwa kuifunga Ingwe, akiwa amefunga katika mechi tatu mfululizo za mashemeji derby.

Kagere aliyejiunga na Simba baada ya kuisaidia Gor Mahia kushinda taji lao la 16 la KPL na Kombe la Sportpesa Super Cup, anaungana na Dan Serunkuma (2012-2013) and Abdul Baraza (1978-1979). Hakuna kama wao.

AFC LEOPARDS NI VIBONDE?

Jibu la hili swali linaweza likapatikana baada ya mechi ya leo. Mpaka sasa wako katika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 48, pointi 20 nyuma ya Gor Mahia kwenye msimamo.

Msimu huu wamepigwa mara tatu. Wamepoteza mashemeji derby tatu za mwaka huu. Walipigwa kwenye mechi ya Hull City Challenge, ESportpesa Super Cup na Ligi Kuu.

WATAKAOKOSA DERBY

Wakati joto la kuelekea mtanange wa leo ukizidi kupanda, taarifa za awali zinasema kuwa, kinara wa mabao wa klabu ya AFC Leopards, Ezekiel Odera, hatacheza mechi ya leo.

Nyota huyo wa zamani wa Gor Mahia, aliyevuka barabara na kujiunga na Ingwe, kutokana na kutumikia adhabu.

Nyota mwengine atakaye kosa mtanange wa leo, ni kinda wa 17, Marvin Omondi Nabwire, Robinson Kamura, Salim ‘Shittu’ Abdalla, Moses Mburu. Ni bahati mbaya sana, kwamba Marvin hatapata fursa ya kuwa mchezaji wa kwanza mwenye umri mdogo zaidi kuwahi kucheza mashemeji derby. 

HISTORIA: DERBY YA KWANZA

Mei 5, mwaka1968, Gor Mahia na AFC Leopards walicheza mechi yao ya kwanza ya mashemeji derby katika uwanja wa City. Katika mchezo huo uliomalizika kwa ushindi wa 2-1, Kogalo wakiondoka uwanjani kidedea, mfungaji akiwa ni William 'Chege' Ouma, huku bao la kufuta machozi la Ingwe likiwekwa kambani na Joe Kadenge mwenyewe.

Katika kikosi chao, Gor Mahia (Luo Nation), walikuwa na James Siang’a, Arthur Omondi, Paul Ndula, Samson Odore, John “Hatari” Owiti, Joseph “Mwalimu” Okeyo, Walter Molo, Steve “McQueen” Yongo, William “Chege” Ouma, John Wambudo na Chris Obure.

Kwa upande Abaluhya Nation (AFC Leopards, walikuwa na Johnstone Tiema, Charles Makunda, Jonathan Niva, Anthony Mukabwa, Moses Wabwai, Daniel Anyanzwa, Joe Kadenge, Livingstone Madegwa, John Nyawanga, John Ambani na Noah Wanyama.

Yote tisa, kumi ni kwamba mechi ya leo, inaweza ikaamua hatma ya ligi msimu hub, kwani Gor Mahia wanahitaji pointi moja tu kutetea taji lao, hata hivyo ni ngumu kutabiri mshindi hasa ukizingatia kuwa wanaokutana ni mashemeji, vita ya mtu na shemeji yake, shahidi ni dimba la Kasarani.