Mashabiki Yanga wapigwa ‘stop’ uwanjani

Friday October 02 2020
yangaa pic

MASHABIKI wawili wa Yanga wanaofahamika kwa majina maarufu ya Osama na Jesca wamefungiwa kuingia uwanjani kwa kipindi cha miezi 12, kwa kosa la kushiriki tukio la kuwapiga na kuwachania jezi mashabiki waliokuwa wamevaa jezi za Simba.

Vurugu hizo zilifanywa wakati Yanga ikicheza na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro ambapo mashabiki walihisiwa kuwa ni wa Simba.

Katika kufanikisha maamuzi hayo picha za mashabiki hao zitabandikwa kwenye mageti yote ya viwanja vinavyotumika kwa michezo ya ligi.

Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) ambayo iliwapa adhabu mashabiki hao pia katika kikao chake cha Septemba 30, 2020 ilipitia mwenendo na matukio mbalimbali yaliyotokea kwenye ligi.

Wakati mashabiki wao wakifungiwa kuingia uwanjani, Yanga yenyewe imetozwa faini ya Sh 500,000 kwa kosa la mashabiki wa timu hiyo waliokuwa upande wa Kaskazini kusukuma geti kwa nguvu na kuingia eneo la kuchezea (pitch) kwa wingi jambo lililopelekea mahojiano kati ya Azam TV na manahodha kukatishwa na kushindikana kuendelea katika mchezo uliochezwa Septemba 27, 2020 kwenye uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.

Yanga wamepewa adhabu hiyo kwa uzingativu wa kanuni ya 45:1 ya Ligi Kuu kuhusu udhibiti wa klabu huku wakipigwa tena faini ya Sh. 500,000  kwa kosa la mashabiki wa timu yake kuonyesha vitendo vya utovu wa nidhamu kwa kuwapiga na kuwachania jezi mashabiki wanaohisiwa ni wa Simba waliovaa jezi za Simba katika mchezo uliochezwa kwenye uwanja huo.

Advertisement

"Kamati inalipongeza Jeshi la Polisi mkoa wa Morogoro kwa kulishughulia jambo hilo kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi.

"Pia kamati inatoa onyo kwa klabu zingine kuelimisha mashabiki wao kutojihusisha na vitendo vyote visivyokuwa vya kimichezo ikiwemo kupigana na kuchaniana jezi," imeeleza taarifa hiyo iliyotolewa na Idara ya Habari na Mawasiliano ya Bodi ya Ligi.

Katika mechi kati ya Kagera Sugar  na KMC ambapo Kagera walishinda bao 1-0, KMC FC imepewa onyo kali kwa kosa la kuchelewa kufika uwanjani ambapo walifika saa 6:42 mchana badala ya saa 6:30 mchana, adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia kanuni ya 15 (54) ya ligi kuu kuhusu taratibu za mchezo.

Vile vile KMC imetozwa faini ya Sh 500,000 kwa kosa la wachezaji wa timu hiyo kutotumia mlango rasmi kuingia uwanjani na badala yake kutumia tundu la uzio wa uwanja kuingilia uwanjani.

Tukio hilo lilifanyika siku moja kabla ya kucheza mechi dhidi ya Kagera Sugar katika Uwanja wa Kaitaba Bukoba, adhabu hiyo imetolewa kwa uzingativu wa kanuni ya 15(15) na 15(54).

Kagera Sugar imetozwa faini ya Sh500,000 kwa kosa la gari aina ya (Noah kuingia uwanjani na kuanza kuzunguka dakika ya tisa ya mchezo na gari aina ya Land Cruiser kuingia uwanjani dakika ya 29 na kuanza kuzunguka uwanjani wakati mchezo ukiendelea mechi iliyochezwa Septemba 25.

Matukio hayo yalitokea kwenye uwanja wa Kaitaba Kagera na adhabu hii imetolewa kwa uzingativu wa kanuni ya 15(15) na 45(1) ya Ligi Kuu kuhusu udhibiti wa klabu.

KONDO NAYE APIGWA 'PIN'

KMC wamepata pigo lingine ukichana na adhabu za timu, kocha msaidizi Habibu Kondo ametozwa faini ya Sh500,000 na kufungiwa michezo mitatu kwa kosa la kuingia uwanjani baada ya mchezo kuisha.

Baada ya kuingia uwanjani Kondo alionekana kuwasumbua waamuzi kwa maneno makali.

Mbeya City imepewa onyo kali katika mchezo waliocheza na Namungo, onyo hilo ni kwa kosa la kuchelewa kufika uwanjani walifika saa 8:54 mchana badala ya saa 8:30 mchana katika mchezo uliochezwa Septemba 25, uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia kanuni ya 15(54).

Pia Mbeya City imetozwa faini ya Sh 500,000 kwa kosa la gari la Mkurugenzi wa Mbeya kuingia uwanjani wakati wachezaji wakiwa wanapasha misuli saa 9:18 mchana.

 

 

 

 

 

 

Advertisement