Mashabiki Simba, Yanga wabadilike

Friday January 11 2019

 

SIMBA kesho Jumamosi itashuka Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, kuikaribisha JS Saoura ya Algeria katika mchezo wao wa kwanza wa Kundi D katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

Hii ni mechi muhimu kwa wawakilishi hao wa Tanzania katika michuano ya kimataifa kwani, ndio mwanzo wa safari yao ya kuelekea kwenye robo fainali kama watafanya vyema mechi zao sote sita za kundi hilo.

Tayari maandalizi kuelekea mchezo huo yameanza tangu mapema wiki hii, ikiwamo kutangazwa kwa viingilio na utaratibu mzima wa mchezo huo wa kimataifa, lakini hata kikosi cha Simba kilichorejea jijini kutoka Zanzibar kinaendelea kujifua.

Simba iliamua kurejesha kikosi chake kutoka kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi ili kujiweka tayari kukabiliana na Waalgeria ambao walitarajiwa kutua usiku wa jana.

Mashabiki wa soka wana hamu kubwa ya kuushuhudia mchezo huo wa kwanza wa Simba, ili kujua hatma na muelekeo wa wawakilishi hao katika safari yao kuisaka tiketi ya robo fainali.

Tunafahamu wapo wanaojiandaa ili kesho wakapata burudani ya soka kutoka kwa timu zote zitakazoumana uwanjani. Wapo wengine wamejipanga kwenye kuipa nguvu Simba kama wawakilishi wa Tanzania, kadhalika wapo watakaoenda Taifa kwa lengo la kuwasapoti JSS kwa kisingizio cha utani wa jadi.

Kama wadau wa michezo, tunapenda kuwakumbusha na kuwahimiza mashabiki wote kuwa, kwa vile Simba ni wawakilishi wa nchi ni lazima wajitokeze kwa wingi kwa

lengo la kuipa nguvu ili ipate matokeo mazuri nyumbani.

Mashabiki uwanjani ni kama mchezaji wa ziada kwa timu wenyeji, hivyo bila kujali ushabiki na itikadi kesho Jumamosi wajitokeze kwa wingi kuishangilia Simba.

Matokeo mazuri ni heshima kwa nchi, hata kama kuna baadhi huyatumia kuwakejeli kwa ule utamaduni wa utani wa jadi. Kufanya vibaya ni hasara kwa Tanzania kwa vile inaiweka pabaya Simba katika mbio zake za kusaka tiketi ya robo fainali. Kushindwa kufuzu kwa Simba katika hatua hiyo ina maana kwamba uwakilishi wa nchi kwa Tanzania utabaki ule ule wa timu moja moja badala ya mbili mbili kama baadhi ya nchi zilizofanikiwa kyufika hatua za juu ya michuano ya CAF.

Tanzania iliyoanza kushiriki michuano hiyo ya Afrika tangu mwaka 1969 ina uwakilishi wa timu moja moja katika michuano ya CAF kwa vile hazijawahi kufika mbali wala kuingia hatua za juu zinazoiongezea klabu zao na nchi pointi za kuwapa upendeleo.

Mataifa kama ya Tunisia, Afrika Kusini, Misri, Algeria, DR Congo, Zambia na mengine ambayo klabu zao zimekuwa zikifanya vizuri kwenye michuano ya CAF zimekuwa na upendeleo wa kuwakilishwa na klabu zaidi ya moja katika kila shindano.

Utazikuta nchi hizo zikiwakilishwa na timu mbili katika Kombe la Shirikisho Afrika na nyingine kama hizo katika Ligi ya Mabingwa Afrika tofauti na nchi zinazotoka kwenye Ukanda wa Afrika Mashariki kwa vile hatujawahi kufanya maajabu.

Hivyo pale panapopatikana nafasi kama inayoshiriki Simba kwa sasa ni sehemu ya Watanzania wote kuungana pamoja kuiunga mkono ili ipate matokeo mazuri katika mechi zao na kufuzu ili kutoa nafasi kwa Tanzania kupendelewa CAF.

Tuliwahi kusema wakati Yanga ilipofika Kombe la Shirikisho mwaka uliopita, lakini ilikuwa ngumu kueleweka ndio maana tunaamua kurudia tena safari hii kwa sababu lengo kama wadau wa michezo na soka kwa ujumla kuona Tanzania tunapiga hatua.

Ushabiki wa kizamani wa kushangilia timu wageni kutoka nje katika mwaka 2019 unapaswa kubaki historia tu. Ndio kwanza tumeanza mwaka na lazima kila kitu chetu kiwe kipya. Mashabiki wawe na fikra mpya kwamba ushabiki uliopitwa na wakati ndio unakwamisha Tanzania kuwakilishwa na timu zaidi ya mbili.

Tunaamini mashabiki wakiwa kitu kimoja, kitasaidia kuwatetemesha wapinzani wa Simba na kuwapa ujasiri hata wachezaji kupambana uwanjani kupata matokeo, kuliko kama watajikuta wakizomewa na kuona wenzao wageni wakishangiliwa kama wapo kwao.

Mashabiki wa soka ni mashahidi wanapoambatana na timu zao kwenda nje ya nchi wanaona namna wenzao wanavyokuwa wa moja, hata kama kuna ushabiki kama uliopo hapa nchini wa Usimba na Uyanga. Wenzao linapokuja suala la kimataifa wanakuwa wamoja na hata kama hawawashangilii wenzao, lakini hawawaungi mkono wageni kwa kujua wageni wataondoka na watabaki kama watu wa taigfa moja.

Simba na Yanga ni timu pinzani, watani wa jadi, lakini sio mahasimu hivyo lazima waonyeshe Utanzania wao kwa kushirikiana pamoja kwenye mechi za aina hii.

Advertisement