Mara Paap! CR7, Mbappe, Neymar ndani ya chama la PSG

PARIS, UFARANSA. LISEMWALO lipo wahenga walisema. Na kama halipo, basi lipo njiani laja. Kwa wiki kadhaa sasa kumekuwa na maneno maneno kwamba supastaa wa Juventus, Cristiano Ronaldo anafikiria kutimkia zake Paris Saint-Germain kwenda kujiunga na mabingwa hao wa Ufaransa katika dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi huko Ulaya.

Ronaldo anaona kama vile maisha huko Juventus yamekuwa magumu, ambapo Ijumaa iliyopita walitupwa nje ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, kisha kocha Maurizio Sarri amefutwa kazi na kuletwa mtu asiyekuwa na uzoefu, Andrea Pirlo kuja kuinoa timu hiyo.

Kinachosemwa kwa sasa ni kwamba wakala wa staa huyo wa zamani wa Manchester United na Real Madrid, Jorge Mendes amepanga kukutana na mkurugenzi wa michezo wa klabu ya PSG kujadili dili hilo, jambo lililodaiwa kuwa gumzo huko Ufaransa. Licha ya janga la virusi vya corona kuripotiwa kuwa na madhara makubwa ya kiuchumi, lakini miamba hiyo ya Ufaransa ipo tayari kulifanya dili hilo kutokea kwa sababu mpango wao ni kuboresha kikosi ndani ya uwanja ili kurudi msimu ujao wakiwa bora zaidi.

Kutokana na hilo, kumeripotiwa kuwa na mazungumzo ya mara kwa mara baina ya Mendes na bosi huyo wa PSG, Leonardo.

Wakala Mendes – ambaye pia amekuwa akimsimamia staa wa Real Madrid, anayesakwa pia na PSG, James Rodriguez, kitu ambacho anapenda kifanyike kwa sasa ni kuhakikisha kwamba dili hilo linakamilika.

Na Le10 Sport linaamini kwamba wawili hao, Mendes na Leonardo wamekuwa wakizungumza kuhusu uhamisho wa Ronaldo baada ya kuona kwamba maisha ya Juventus yamekuwa na changamoto nyingi.

Ripoti zinadai kwamba PSG watatumia nafasi ya kwenda kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya huko Ureno kama fursa ya kukutana na Ronaldo, kwa sababu kwa wakati huu mchezaji huyo atarejea mapumziko kwao baada ya kumalizika kwa msimu wa Serie A.

Ronaldo, 35, alijiunga na Juventus miaka miwili iliyopita na kusaini mkataba wa miaka minne, ambapo kwa sasa amebakiza miwili ya kuendelea kubaki kwenye kikosi hicho cha wababe wa Turin.

Licha ya kuvunja rekodi kadhaa huko Serie A na kuipa Juventus ubingwa wa ligi, msimu huu umekwisha na mambo mengi kibao ya kuhuzunisha na hivyo kufikiria kuachana na timu hiyo. Kipigo kwenye mechi za fainali za Suppercoppa Italiana na Coppa Italia vilifuatia na kutupwa nje Ligi ya Mabingwa Ulaya na Lyon Ijumaa iliyopita kulitibua mambo na kumfanya kocha Sarri atimuliwe.

Na sasa Ronaldo anafikiria hatima yake ya baadaye wakati huu akienda zake likizo na mchumba wake, mrembo Georgina Rodriguez.

Staa huyo kwenye posti yake ya Instagram aliyotuma Jumamosi iliyopita, aliandika maneno haya: “Msimu wa 2019/20 umeshakwisha kwa upande wetu, kwa kuchelewa sana kuliko kawaida, lakini kwa haraka kuliko ilivyotarajiwa.

“Sasa ni muda wa kutafakari, kufikiria mapito yote kwa sababu hiyo ndiyo njia pekee ya kuboresha mambo.

“Pengine hiki kipindi kifupi cha likizo kitaturuhusu kufanya uamuzi sahihi wa mambo ya baadaye na kurudi tukiwa na nguvu mpya na majukumu makubwa kuliko ilivyokuwa mwanzo.”

Ripoti za wiki iliyopita zilidai kwamba Ronaldo hafurahii maisha huko Juventus na kwamba alikaribia kabisa kutua PSG kabla ya kuibuka kwa janga la corona.