Manji 'amrejesha' Chirwa Jangwani

Muktasari:

Chirwa msimu uliopita alikuwa mfungaji bora wa Yanga baada ya kufunga mabao 12 katika Ligi Kuu Bara

Dar es Salaam.Siku chache tangu ifahamike bilionea na Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji amerejea rasmi, mashabiki wa klabu hiyo jioni hii wamefanyiwa 'sapraizi' baada ya kumshuhudia nyota wao wa zamani, Obrey Chirwa akiwa Uwanja wa Taifa.

Chirwa ameibuka Uwanja wa Taifa wakati Yanga ikivaana na Alliance ya Mwanza na kuwapa shangwe mashabiki ambao bado wanaukubali mchango wa Mzambia huyo aliyetimkia Misri baada ya mkataba wake na klabu hiyo kumalizika.

Chirwa aliyeifungua Yanga jumla ya mabao 24 katika msimu yake miwili ya kucheza Ligi Kuu akiwa na klabu hiyo ameonekana uwanjani hapo akiwa jukwaani huku akifuatilia kwa ukaribu mpambano huo ambapo Yanga ipo mbele hadi sasa.

Chirwa na Abass Talimba walifika uwanjani hapo dakika 37 na kukaa VP A, kitendo kilichowafanya mashabiki kuacha kuangalia mechi kama dakika 2 hivi wakimshangilia.

Badaae mashabiki hao walimtaka Chirwa asimame ili awapungie mkono naye Straika huyo hakusita kufanya hivyo.

Chirwa alipunga mikono yake iliyofanya vifijo na kelele za mashabiki kutawala kwa muda mfupi mpaka alipokaa.

Tambo zilianza kwa mashabiki wa Yanga wakidai amekuja kiboko wa beki ya Simba kama Pascal Wawa, Mohammed Hussein "Tshabalala" na wengine.

Mabao ya Heritier Makambo katika dakika 17 na lingine la Mrisho Ngassa dakika ya 24 yameifanya Yanga kuwa mbele hadi sasa kwa magoli 2-0, ikiwa ni mchezo wa kwanza tangu ifahamike Manji aliyetangaza kujiuzulu Uenyekiti Mei 20 mwaka jana kugomewa na wanachama na kurejea klabu ili kuendelea na cheo chake.

Kamati ya Uchaguzi Mkuu ya Yanga, ilitangaza uchaguzi mdogo wa klabu hiyo kwa kutangaza nafasi za Makamu Mwenyekiti na nyingine tatu za Wajumbe wa Kamati ya Utendaji utakaofanyika Novemba 24.