Breaking News
 

Man United yaambiwa dau la Dybala ni zaidi ya Coutinho

Friday January 12 2018

 

TURIN, ITALIA

MAMBO ni moto. Manchester United wameambiwa hivi kama kweli wapo 'siriazi' wanamtaka kumsajili Paulo Dybala basi itabidi wajipange, waende na pesa inayozidi ile waliyotumia Barcelona kumsajili Philippe Coutinho kutoka Liverpool, ripoti inafichua.

Mbrazili, Coutinho alihama kutoka Liverpool hadi Barcelona kwa ada ya Pauni 145 milioni na hivyo kuwa mwanasoka ghali namba tatu duniani, lakini uhamisho wake ukiweka rekodi England kwa kuwa mchezaji aliyeuzwa kwa pesa nyingi zaidi.

Kwa mujibu wa gazeti la Italia, Tuttosport, uhamisho huo wa pesa nyingi wa Coutinho umezidi kuzua kizaazaa huko Turin na Juventus sasa itakitumia kama kigezo katika kufanya mazungumzo yoyote yanayohusiana na mpango wa kumpiga bei staa wao, Dybala.

Si unajua kwamba kwenye Serie A msimu huu, Ciro Immobile na Mauro Icardi peke yao ndiyo waliofunga mara nyingi kuliko Dybala, hivyo Juventus wanatumia hiyo kama fimbo pia ya kuwachapa wanaojifanya wanahitaji saini ya mchezaji huyo.

Kwa muda sasa, Dybala amekuwa akihusishwa na mpango wa kuhamia Man United wakimchukulia kama mbadala kufuatia Antoine Griezmann kuweka masharti ya kutaka kulipwa mshahara wa Pauni 400,000 kwa wiki ili atue Old Trafford.

Man United wanaamini Dybala atakwenda kutengeneza kombinisheni nzuri ya ushambuliaji sambamba na Romelu Lukaku, wakati Paul Pogba, ambaye amekuwa akifahamika kwa jina la utani la ‘Agent P’ akipiga ndogo ndogo ili staa mwenzake huyo wa zamani wa Juventus atue Manchester.

Lakini, katika kulifanya hilo kutimia, Man United itabidi kutoboa mfuko. Man United ya Jose Mourinho ilitumia pesa nyingi pia kumnasa Pogba wakati ilipomng'oa kwa vibibi vizee hivyo vya Turin kwa ada ya uhamisho ya Pauni 89 milioni na kuvunja rekodi kwa wakati huo kabla ya uhamisho wa Neymar, Ousmane Dembele, Coutinho na wengine akiwamo Kylian Mbappe aliyekopwa kwa Pauni 168 milioni huko PSG, ambapo pesa hizo zitalipwa AS Monaco mwishoni mwa msimu.