Ronaldinho: Mambo matano ya kukumbukwa akitimiza miaka 40 gerezani

Tuesday March 24 2020

Mambo matano ya kukumbukwa akitimiza miaka 40 gerezani,Ronaldino gerezani huko Paraguay,ronaldino akamatwa na pasipoti feki paraguay,ronaldino kusota jela,Mwanasport,

 

ASUNCION, PARAGUAY . HAJAPATA kutokea na hatatokea tena. Yaani kuna Ronaldinho mmoja tu na itabaki kuwa hivyo. Gaucho ni mmoja na hatotokea mwingine kama yeye. Kwa bahati mbaya sana kwa sasa yuko gerezani huko Paraguay, ambako ameshitakiwa kwa kosa la kumiliki hati feki ya kusafiria ya nchi hiyo. Huyo ni Gaucho, na akili zake ndivyo zilivyomtuma.

Kwa walioshuhudia udambwidambwi wake uwanjani, wanaofahamua na kufuatilia historia ya maisha yake, hakika haishangazi kabisa kwa staa huyu kusherehekea siku yake ya kuzaliwa akiwa gerezani. Hana tena uhuru wa kula bata na warembo na kusafiri kwa kadri anavyotaka.

Amefanya mambo mengi katika historia ya maisha yake na sasa huko gerezani anaendelea kuburudisha wafungwa wenzake.

Nyota huyu wa zamani wa Barcelona na AC Milan, wiki iliyopita akiwa gerezani anakozuiliwa kwa miezi sita, alitimiza miaka 40 ya kukaa kwenye uso wa dunia. Lakini, wakati akisubiri hatima yake si vibaya tukakumbuka mambo yake japo kwa uchache tu.

Kuwaliza Waingereza- Kombe la Dunia (2002)

Hivi alimaanisha kufanya vile au ilikuwa bahati mbaya? Hii itabaki kuwa siri yake na Mungu wake. Ni ngumu kujua kama alidhamiria kumfanya vile David Seaman au la. Lakini kwa kauli yake mwenyewe, Ronaldinho ameendelea kusisitiza ile free-kick alidhamiria.

Advertisement

Ilikuwa ni katika mchezo wa robo fainali ya Kombe la Dunia mwaka 2002. Juni 21, 2002, katika dimba la Shizuoka, Ronaldinho aliishangaza dunia. Mabao mawili kutoka kwa Ronaldo de Lima na Gaucho yaliwaliza Wajukuu wa Malkia. Lakini bao ambalo liliwaliza zaidi ni la Gaucho, liliwaliza zaidi bao tamu

England ikiwa na matumaini ya kusawazisha bao la Ronaldo, Brazil ilipata free-kick na Ronaldinho akateuliwa kutoa hukumu dhidi ya Seaman. Ngome ikapangwa vizuri na baada ya kujiaminisha kila kitu kiko sawa Seaman alishuhudia tu mpira ukimpita utosini.

Mashuti ya mbali-2003

Dunia inamkumbuka Ronaldinho kutokana na uwezo wake mkubwa wa kupiga chenga za maudhi na akili nyingi anapokuwa na mpira mguuni, lakini tusisahau kuwa mchawi huyu wa soka aliyetokea Porto Allegre, alikuwa bingwa wa kufunga mabao kwa shuti kali.

Katika mchezo wa La Liga dhidi ya Sevilla mwaka 2003, aliuchukua mpira akiwa katikati ya uwanja, akapiga densi zake na kuwapiga wachezaji kadhaa wa Sevila, kabla ya kuachia shuti kali lililotinga wavuni akiwa umbali wa yadi 30.

Kocha wa Barcelona wakati huo, Frank Rijkaard alijikuta akirudi kwenye benchi, mikono kichwani asiamini alichokiona kutoka kwa kiungo wake huyo, ambaye alihisi anaujua uwezo wake wote akifanya maajabu mengine, kwa mguu wake wa kulia.

Maajabu ya Stamford Bridge-2005

Ukipepesa jicho lako tu limekupita. Hivyo ndivyo maajabu ya Stamford Bridge yalivyotokea. Kama kuna kitu cha ajabu ambacho amewahi kukifanya katika maisha yake ya soka, ni hiki alichomfanyia Jose Mourinho na vijana wake pale Darajani.

Chelsea walikuwa wanaongoza kwa matokeo ya jumla ya mabao 4-3 katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya hatua ya 16 bora. Lakini, hawakujua kuna mtu anaitwa Ronaldinho na alikuwa bado hajafanya alichokifanya na kuifanya dunia isimame kwa sekunde kadhaa kwa heshima yake.

Akiwa na mpira mguuni ndani ya boksi ya Chelsea na mbele yake akitazamana na mabeki watatu, John Terry, Ricardo Carvalho na Ashley Cole. Alijitikisa mara ya kwanza (kulia) na ya pili (kushoto) kabla ya kuubetua mpira juu ukaenda moja kwa moja wavuni.

Bao hilo ambalo hata hivyo halikutosha kuipatia Barca ushindi (walipigwa 5-4) lilimshangaza hadi yeye kwani alichukua muda kidogo kabla ya kushangilia. Kipa wa Chelsea Petr Cech aliishia kuushangaa tu mpira unavyokwenda nyavuni.

Aliiteka Santiago Bernabeu-2005

Ukiona mashabiki wa timu pinzani wakiinuka vitini na kumshangilia mchezaji wa timu pinzani basi ujue kuna jambo lisilo la kawaida. Hapa namzungumzia Gaucho, ambaye alisimamisha Santiago Bernabeu kwa heshima na mashabiki wakasahau ni mchezaji wa timu pinzani.

Katika mchezo wa El Classico ambao Barcelona wakiwa wanaongoza 1-0 likifungwa na Samuel Eto’o. Ronaldinho alifunga ukurasa kwa mabao mawili ya hatari. Bao la kwanza, alianza kukimbia akitokea upande wa kushoto mwa uwanja akimpita Sergio Ramos kwa kasi.

Baada ya hapo akahamia katikati ya uwanja, akaingia ndani ya boksi na hakuchelewa sana akapiga shuti la chini lililomwacha Iker Casillas, akishangaa tu asijaribu hata kujirusha.

Bao la pili akafanya vile vile tena kwa kasi ile ile, alimpita Ramos kabla ya kubetua mpira uliompitia Casillas kichwani.

Kilichofuata ni mashabiki wa Real Madrid kusimama kwenye viti vyao (Spontaneous Standing Ovation). Tukio hili lilimpatia tuzo lake la pekee la Ballon d’Or.

Bao la ndoto zake- tiki taka (2006)

Katika msimu wake wa mwisho pale Camp Nou akiwa ameshaanza kuonyesha kushuka kiwango. Ronaldinho aliendelea kuonyesha uwezo aliojaaliwa miguuni.

Ni wakati huu, ndipo alipotimiza ndoto ya maisha yake, japo kwa kuchelewa.

Mpira ulipigwa kutoka winga ya kushoto na kiungo maestro, Xavi Hernandez, Gaucho akaupokea bila hofu na kuutuliza kifuani ukashuka chini kidogo, akabinuka na kuachia tiki-taka iliyotinga nyavu za juu huko anakotaga ndege.

Baada ya mechi hiyo kumalizika (walikuwa wanacheza dhidi ya Villarreal), alisikika akisema:

“Tangu nikiwa mdogo nilikuwa na ndoto ya kufunga bao la aina hii, sasa inabidi nijaribu kutimiza ndoto yangu nyingine, ambayo ni kufunga kutoka katikati ya uwanja.”

Advertisement