Makocha wanaolipwa mishahara mikubwa kwa wiki

Muktasari:

Lakini, ushawahi kujiuliza makocha wanaowanoa mastaa hao wanaolipwa mikwanja mirefu kila wiki wao wanalipwa kiasi gani cha pesa kwenye wiki hizo.

Cheki hapa, makocha 10 duniani wanaolipwa mishahara mikubwa kwa wiki.

LONDON, ENGLAND . STAA, Raheem Sterling yupo kwenye mazungumzo ya kunasa dili jipya huko Manchester City ambalo litamfanya awe mchezaji anayelipwa pesa nyingi kuliko yeyote huko Etihad. Anaripotiwa kwamba dili hilo mpya litamfanya Sterling alipwe Pauni 450,000 kwa wiki.

Lakini, ushawahi kujiuliza makocha wanaowanoa mastaa hao wanaolipwa mikwanja mirefu kila wiki wao wanalipwa kiasi gani cha pesa kwenye wiki hizo.

Cheki hapa, makocha 10 duniani wanaolipwa mishahara mikubwa kwa wiki.

10. Jurgen Klopp (Pauni 134,615 kwa wiki)

Baada ya kuwapa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, Liverpool huwaambii kitu kuhusu kocha wao Mjerumani, Jurgen Klopp. Huduma yake bora anayotoa huko Anfield ilimfanya awindwe na klabu kadhaa za huko Ulaya, lakini Liverpool wanapambana kwa kila hali kuhakikisha anabaki, ikiwezekana kumpa mshahara mkubwa zaidi, ambapo kwa sasa analipwa Pauni 7 milioni kwa mwaka. Lakini, mkwanja huo unaingia kwenye akaunti ya Klopp kila wiki, Pauni 134,615.

9. Ernesto Valverde (Pauni 153,846 kwa wiki)

Barcelona ni moja ya timu ambazo zimeingia kwenye orodha ya klabu 10 Ulaya zinazowalipa mishahara mikubwa makocha wao. Wababe hao wa Nou Camp wananolewa na Ernesto Valverde, ambaye kwa kila mwaka wanamwingizia kwenye akaunti yake ya benki, Pauni 8 milioni. Kocha huyo aliyepata bahati ya kumnoa staa wa dunia, Lionel Messi jambo hilo linaendana na mshahara wake ambapo kwa kila wiki anavuna Pauni 153,846. Si pesa ya mchezomchezo.

8. Thomas Tuchel (Pauni 153,846 kwa wiki)

Kwa kocha yeyote anapoambiwa kwamba anatafutwa na Paris Saint Germain bila ya shaka atakuwa mwenye furaha kubwa kwa sababu anafahamu wazi anakwenda kuchukua kazi ya pesa ndefu. Si unajua timu hiyo inamilikiwa na matajiri wa Kiarabu, hivyo suala la kulipwa mshahara mkubwa sio tatizo na kocha Tuchel kwa mwaka anaweka mfukoni Pauni 8 milioni. Tuchel yupo vizuri, kwenye akaunti yake ya benki inaingizwa mshahara wa Pauni 153,846 kwa wiki.

7. Antonio Conte (Pauni 173,077 kwa wiki)

Conte alipofutwa kazi huko Chelsea, alikaa kijiweni kwa muda kidogo kabla ya kwenda kuikamatia kazi ya kuinoa Inter Milan. Ajira hiyo iliyomrudisha kwao Italia, imemfanya Conte kutokuwa na maisha ya kinyonge kwa sababu mshahara wake anaolipwa ni mzuri, Pauni 9 milioni zinaingia kwenye akaunti yake ya benki kwa mwaka. Lakini, kitu kitamu zaidi kwake ni kwamba mkwanja huo analipwa ka kila wiki, ambapo ndani ya siku hizo saba, Conte anaweka mfukoni Pauni 173,077.

6. Zinedine Zidane (Pauni 192,308 kwa wiki)

Zinedine Zidane alikuwapo Real Madrid kama mchezaji, kisha akawa kocha na kuondoka na baadaye kurudi tena kuchukua mikoba ya kuinoa timu hiyo. Kocha huyo Mfaransa hakurudi Bernabeu kinyonge, akiwa kwenye orodha ya makocha wanaofurahia kazi zao kutokana na kulipwa mishahara ya kibosi. Kwa mwaka kocha huyo analipwa Pauni 10 milioni. Zidane mambo yake si mabaya, akaunti yake ya benki inanona si mchezo, akilipwa Pauni 192,308 kwa wiki.

5. Fabio Cannavaro (Pauni 192,308 kwa wiki)

Unamkumbuka Fabio Cannavaro? Yule beki kisiki wa zamani Mtaliano aliyewahi kuchaguliwa kuwa mwanasoka bora wa dunia wa mwaka. Kwa sasa ni kocha wa Guangzhou Evergrande ya China. Ajira huyo inamfanya Cannavaro kuwa kwenye orodha ya makocha watano wanaolipwa pesa nyingi duniani, ambapo kwa mwaka akavuna mshahara wa Pauni 10 milioni. Cannavaro analipwa vizuri kuliko makocha PSG, Barcelona na Inter Milan, Pauni 192,308 kwa wiki.

4. Rafael Benitez (Pauni 221,154 kwa wiki)

Haikumfanya Rafa Benitez kuwa na mawazo mengi kuchukua uamuzi wa kuachana na Newcastle United na kwenda kujiunga na Dalian Yifang ya China. Kishawishi kikubwa ni pesa. Kwenye ajira yake hiyo ya huko China, Benitez kwa mwaka analipwa Pauni 11.5 milioni. Lakini, ukiona mwaka ni mkubwa sana, kila wiki Mhispaniola huyo aliyeamua kuachana na ubabaishaji wa Mike Ashley huko Newcastle, kwenye akaunti yake ya benki kila wiki inaingizwa Pauni 221,154.

3. Diego Simeone (Pauni 250,000 kwa wiki)

Aliposaini dili jipya la kuendelea kubaki Atletico Madrid wengi walimshangaa Diego Simeone wakiamini kwamba ulikuwa wakati mzuri wa kwenda kwenye timu nyingi baada ya kile alichokifanya kwenye kikosi hicho cha Wanda Metropolitano. Lakini, mkwanja ndio uliomfanya Muargentina huyo kubaki an Atletico, kulipwa Pauni 13 milioni kwa mwaka si pesa ndogo, huku kila wiki akiwa analipwa mshahara Pauni 250,000. Angewezaje kuondoka kirahisi tu.

2. Jose Mourinho (Pauni 288,462 kwa wiki)

Jose Mourinho amenasa ajira mpya kwa sasa baada kuchukua mikoba ya kuinoa Tottenham Hotspur, ikiwa karibu mwaka tangu alipofutwa kazi huko Manchester United. Ajira yake mpya huko Spurs si haba, kwani imemfanya kocha huyo kuwa kwenye orodha ya wanaolipwa vizuri, akivuna Pauni 15 milioni mwaka na kila wiki akaunti yake ya benki inanona, Pauni 288,462 zinaingizwa. Mourinho ametua Spurs akiwa na jukumu moja la kuanza kuipa timu hiyo mataji.

1. Pep Guardiola (Pauni 384,615 kwa wiki)

Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola ndiye mwenye dili tamu zaidi kuliko makocha wote wanaotamba barani Ulaya kwa sasa.

Huduma yake anayotoa huko Etihad, inamwingiza Pauni 20 milioni kwa mwaka huu, kila wiki kocha huyo Mhispaniola kwenye akaunti yake ya benchi inaingia Pauni 384,615. Man City wanapesa na hivyo wameona njia nzuri ya kupata huduma bora kutoka kwa kocha mkubwa kabisa ni kumlipa mshahara mkubwa. Habari ndiyo hiyo.