Makocha wamchana Bernard Morrison, waifagilia Simba

Tuesday July 14 2020

 

By Oliver Albert

Dar es Salaam. Makocha wameipongeza Simba kwa kiwango ilichoonyesha dhidi ya Yanga katika mchezo wa Kombe la Shirikisho (FA) juzi, lakini wamelaani kitendo cha utovu wa nidhamu kilichoonyeshwa na mshambuliaji wa Yanga, Benard Morrison ambaye aligomea kukaa benchi na kutokomea kusikojulikana.

Katika mchezo huo uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Yanga ililala kwa mabao 4-1.

Kutokana na mchezo ulivyokuwa katika dakika ya 64 Kocha wa Yanga, Luc Eymael alifanya mabadiliko kwa kumtoa Morrison na kumuingiza Patrick Sibomana, lakini mshambuliaji huyo aliyeifunga Simba kwenye mchezo wa Ligi Kuu uliochezwa Machi 8 aligoma kukaa benchi kama sheria na kanuni za soka zinavyotaka.

Baada ya kutoka uwanjani Morrison alipita nyuma ya benchi la wachezaji wa akiba na makocha wa Yanga, na kuelekea vyumbani, lakini hata pale mwamuzi wa akiba Nadeem Alyoce alipomkimbilia na kumtaka kurejea kwenye benchi alijikuta akisukumwa na kuàmua kuachana naye.

Jambo hilo lilionekana kuwakera hata mashabiki wa Yanga ambapo wakati akienda vyumbani walisikika wakimzoea.

Makocha, wadau wa soka

Advertisement

Akizungumzia mchezo huo, kocha wa Biashara United, Francis Baraza alisema Simba ilikuwa bora kila eneo na ilistahili kushinda.

“Walikuwa katika kiwango bora kwenye maeneo yote uwanjani,” alisema Baraza huku akisisitiza kuwa katika kikosi cha Yanga mchezaji aliyetisha ni Feisal Salum ‘Fei Toto’.

“Licha ya kwamba Yanga ilijaza viungo wengi katikati, lakini Simba walipita hapohapo katikati kwa sababu viungo wa Yanga walioongozwa na Papy Tshishimbi, Haruna Niyonzima, Fei Toto walikuwa wazuri wakiwa na mpira lakini wasipokuwa nao walikuwa mzigo kwa timu.”

Kuhusu Morrison, Baraza alisema: “Amefanya kitendo kibaya sana na kama mimi ndiye ningekuwa kocha wa Yanga, basi ndio ungekuwa mwisho wake. Yeye ni mchezaji hana haki ya kupinga uamuzi unaofanywa na benchi la ufundi.”

Naye kocha wa Prisons, Adolph Rishard alisema Morrison hana nidhamu na angekuwa kocha wake asingemvumilia.

“Mchezaji kama huyo wa nini kwenye timu. Yaani timu imefungwa, halafu unatolewa unafanya kitendo kile cha utovu wa nidhamu, yaani siku hiyohiyo utaondoka,” alisema Rishard.

Namungo yaivulia kofia Simba

Kocha wa Namungo FC, Hitimana Thiery aliyekuwepo uwanjani kuangalia pambano hilo la watani wa jadi alikiri kuwa Wekundu wa Msimbazi walikuwa bora zaidi.

Hitimana ambaye timu yake imeingia fainali ya FA kwa kuichapa Sahare All Stars ya Tanga bao 1-0, aliongozana na wachezaji wake katika mchezo huo ili kuwasoma Simba watakaokutana nao katika fainali itakayofanyika Agosti 2 mjini Sumbawanga mkoani Rukwa.

“Mpira ambao Simba wanacheza kwa sasa ni lazima tukubali wako juu sana, nawapa hongera kwani hawakuifunga Yanga kibahati. Mchezo wa fainali baina yetu utakuwa mzuri, lakini nikiri nina kibarua kikubwa kutokana na Simba walivyo katika ubora, ila tutapambana kuona jinsi gani tunatwaa ubingwa,” alisema.

Advertisement