Makocha: Ligi bado mbichi

Wednesday September 16 2020

 

By Majuto Omary

Kocha Mkuu wa timu ya Ruvu Shooting, Charles Boniface Mkwasa amesema kuwa ni mapema sana kutabiri kuwa timu zinazoongoza ligi kuu kuwa zitamaliza katika nafasi hizo hizo na kutwaa ubingwa.

Timu ya KMC ndiyo ipo kileleni kwa tofauti ya mabao ya kufunga baada ya kukusanya jumla ya pointi sita. Imeshinda mechi mbili, dhidi ya Mbeya City kwa mabao 4-0 na Tanzania Prisons kwa mabao 2-1.

Azam FC inashika nafasi ya pili kwa kuwa na pointi sita kufuatia ushindi wa nyumbani wa bao 1-0 dhidi ya Polisi Tanzania na 2-0 dhidi ya Coastal Union.

Nafasi ya tatu wapo Dodoma Jiji FC imekusanya pointi sita kwa kushinda 1-0 dhidi ya Mwadui na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya JKT Tanzania.

Kwa mujibu wa Mkwasa, ushindani umekuwa hata kwa wachezaji wa ndani dhidi ya kigeni ambapo mpaka sasa wachezaji Hassan Kabunda wa KMC na Mzamiru Yasin wa Simba wamefunga mabao mawili kila mmoja huku mfungaji bora wa msimu uliopita, Meddie Kagere akiwa hajafunga mpaka sasa.

Mshambuliaji mpya wa azam FC, Prince Dube ndiye amefunga mabao mawili kwa wachezaji wa kigeni.

Advertisement

Wachezaji wengine wa kigeni ambao wamefunga bao moja kila mmoja ni Michael Sarpong,Lamine Moro(Yanga),Emmanuel Mvuyekule(KMC) Boban Zirintusa (Mtibwa Sugar), Obrey Chirwa (Azam) na Bigirimana Blaise wa Namungo FC.

“Nani alitarajia upinzani ambao Mbeya City imeuonyesha dhidi ya Yanga na Mtibwa Sugar dhid ya Simba. Hii ni ishara kuwa msimu huu ni mgumu sana kulinganisha na misimu iliyopita.

Kuna mwamko mkubwa sana wa wachezaji wa nyumbani dhidi ya wale wa kigeni, hii ni changamoto na ninaamini hali itakuwa ngumu zaidi kwa kadri ligi inavyoendelea,” alisema Mkwasa ambaye timu yake imetoka sare mechi moja na kufunga moja.

Kocha Mkuu wa timu ya KMC, Habib Kondo alisema kuwa safari hii wamejipanga kufanya vyema katika ligi tofauti na msimu uliopita.

 

 

Advertisement