Maka: FDL ngumu asikuambie mtu

SIKU moja baada ya kuiwezesha Ihefu SC kupanda kucheza Ligi Kuu msimu ujao, kocha wa kikosi hicho, Maka Mwalwisi amesema Ligi Daraja la Kwanza (FDL) ngumu na inachangamoto nyingi.

Maka amesema moja ya changamoto kubwa zinazoikabili ligi hiyo ni kuwapo kwa timu nyingi ambazo hazina uchumi mzuri unaowasaidia kutekereza mahitaji yao kwa nyakati sahihi.

"Nimefundisha timu nyingi za FDL, ikiwemo Mbeya City, Mlale FC na Mbeya Kwanza na changamoto ya uchumi imekuwa ikitukwamisha na kufanya vitu katika mazingira sio rafiki.

'Unasafiri na timu usiku mzima halafu asubuhi mnapumzika ili jioni mkacheze hali ambayo wengi wanaingia uwanjani wakiwa wamechoka," amesema Mwalwisi.

Ameongeza hali hiyo inatokana na timu hizo kukosa udhamini pamoja na ligi yenyewe kukosa udhamini na kujikuta ikijiendesha kwa mazingira ya kutegemea zaidi pesa za mifukoni.

Maka, jana aliiwezesha Ihefu SC kupanda Ligi Kuu baada ya kuitoa Mbao FC katika mchezo ya hatua ya mtoano licha ya kufungwa mabao 4-2 hivyo ikiwa na faida nzuri ya mabao ya ugenini baada ya nyumbani kushinda 2-0.

Kwenye msimamo wa Kundi A ambalo Dodoma Jiji iliongoza na kupanda moja kwa moja, wote walimaliza na alama 51.