Majeraha yamtibulia straika Kagera Sugar

Muktasari:

  • Frank alipata majeraha ya goti katika mechi ya Yanga dhidi ya Kagera Sugar uliochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Januari 15.

STRAIKA Frank Hamis wa Kagera Sugar amesema majeraha ya goti aliyoyapata katika mchezo wao dhidi ya Yanga uliochezwa Februari 15, yamemfanya ashindwe kuvuka idadi ya mabao aliyopachika msimu uliopita akiwa na Mbeya City.

Frank akiwa na Mbeya City msimu uliopita alifunga mabao sita, lakini msimu huu hadi sasa ameifungia matatu tu.

Akizungumza na Mwanaspoti alisema, changamoto ya majeraha imepelekea akose idadi kubwa ya mechi njambo lililomfanya ashindwe kutimiza lengo alilojiwekea.

"Sijacheza mechi nyingi kwa sababu niliumia goti tangu mchezo wetu na Yanga, pia katika raundi ya kwanza nimecheza mechi tisa, baada ya kuumia mpaka hivi sasa tunavyo zungumza bado nipo nje," alisema mshambuliaji huyo.

Hamis alisema kwa sasa amekubali yaishe kwani anatarajia kurejea uwanjani mwishoni mwa msimu.

"Naweza kurejea katika mechi tatu za mwisho hapo ndio nimeambiwa nitakuwa sawa, kwa hiyo nasubiri kuangalia hali yangu itakavyokuwa.

Majeraha hayajakatisha ndoto zangu kwa sababu mimi bado ni kijana mdogo na naweza kurejea, naweza kusema tu nimekuwa na msimu mbaya sijaweza kufanya kile nilichokuwa nimekitarajia lakini nina imani nitarudi na nitafanya makubwa," alisema Hamis.

Licha ya kukosekana mshambuliaji huyu, Kagera Sugar msimu huu wamekuwa wakibebwa vilivyo na nyota wao mwingine, Yusuph Mhilu ambaye ameifungia mabao  11 hadi sasa.