Mageuzi Ligi Kuu England

London, England. Mwenyekiti wa Ligi ya England, Rick Parry amezisifu klabu za Liverpool na Manchester United kwa ‘kuonyesha uongozi’ baada ya kuibuka na mpango wa kufanya mageuzi makubwa ya Ligi Kuu, ambayo anaamini yataunufaisha mchezo huo.

Mpango huo tata wa ‘Project Big Picture’ (Mradi wa Mtazamo Mpana) unajumuisha mapendekezo ya kupunguza timu za Ligi Kuu kutoka 20 hadi 18 na kufuta michuano ya Kombe la Ligi na mechi ya Ngao ya Jamii.

Klabu itakazomaliza msimu ikishika nafasi ya 16 katika Ligi Kuu itaingia katika michuano ya mtoano pamoja na timu za daraja la kwanza, wakati kutakuwa na haki pana zaidi za kupiga kura kwa klabu tisa zilizocheza Ligi Kuu kwa muda mrefu.

Chini ya mpango huo, klabu za Ligi Kuu zitapata Pauni 250 milioni za Kiingereza (sawa na zaidi ya Sh755 bilioni za Kitanzania) na asilimia 25 ya mapato yajayo ya Ligi Kuu kwa mwaka.

Mechi za soka nchini England zimekuwa zikichezwa bila ya mashabiki tangu mwezi Machi kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya corona, Covid-19 na klabu za ligi za chini zimekuwa zikikabiliwa na tatizo kubw ala kifedha kutokana na mashabiki kuzuiwa kuingia viwanjani.

Parry alisisitiza kuwa pendekezo hilo -- ambalo litasababisha mabadiliko makubwa kuwahi kutokea kwa kizazi hiki -- yanatoa nafasi bora ya hali ya baadaye kwa klabu zilizo nje ya Ligi Kuu, lakini yamekuwa na ubaguzi.

Ligi Kuu ilisema mpango huo utakuwa na “na athari mbaya kwa mchezo mzima” wakati idara ya Digital, Utamaduni, Habari na Michezo iliponda kile ilichokiita “mipango ya pembeni”.

Liverpool, Man Utd zasifiwa

Lakini Parry, mtendaji mkuu wa zamani wa Liverpool na Ligi Kuu, alikuwa amejaa sifa kwa Liverpool na United, klabu mbili zenye mafanikio makubwa.

“Ni klabu mbili kati ya kubwa zilizoonyesha uongozi wakati zinapotakiwa kufanya hivyo, zikionyesha uwajibikaji mkubwa, na kwa mtazamo wa Ligi Kuu, mpango huo unazifanya klabu zetu kuwa endelevu na kupunguza tofauti kati ya timu zilizo juu katika Ligi Daraja la Kwanza na zilizo mkiani mwa Ligi Kuu,” alisema Perry.