Magari viwanjani mechi zikiendelea hatari tupu

Muktasari:

  • Sasa wakati mchezaji anataka kuhema apate hewa ya kutosha, ndipo magari yanaingia uwanjani yakitoa moshi mzito na kutimua vumbi.

MIAKA ya zamani, kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam (siku hizi Uwanja wa Uhuru), magari yalikuwa yakiingia na kupiga misele ndani wakati michezo ikiendelea, watu walishangilia.

Lakini kwa sasa, hiyo ni zilipendwa, kwani hali kama hiyo imebaki kwenye viwanja vya mikoani kama Mbeya, Mwanza na Shinyanga, kuvitaja kwa uchache.

Huku mechi inaendelea, linaingia lori kubwa limebeba askari halafu linatimua vumbi huku likitoa moshi mwingi...hii si sawa!

Kitaalam, mtu anapokimbia sana au anapofanya shughuli inayotumia nguvu nyingi, huongeza kiwango cha kuhema.

Hii ni kwa sababu anakuwa ametumia hewa nyingi mwilini mwake, hivyo hulazimika kuivuta nyingine kutoka nje ili kulipa lile deni la hewa mwilini...ndipo huhema kwa haraka haraka sana.

Michezo, mpira ukiwemo, ni moja ya kazi zinazomlazimu mchezaji kutumia hewa nyingi ya mwilini hivyo kuhitaji hewa nyingine kutoka nje.

Sasa wakati mchezaji anataka kuhema apate hewa ya kutosha, ndipo magari yanaingia uwanjani yakitoa moshi mzito na kutimua vumbi.

Hapo mchezaji badala ya kuvuta hewa safi, huvuta ule moshi na vumbi na kuhatarisha afya yake.

Usiombee moja ya timu zinazocheza, iwe ya jeshi. Yatakuja malori yamebeba vijana wa JKT yakiendeshwa kwa mbwembwe za hali ya juu huku abiria walipiga mayowe kuonesha ujasiri wao.

Mara utaona msafara wa mkuu wa mkoa unaingia uwanjani.

Magari kuingia uwanjani inaweza isiwe tatizo, lakini kuingia wakati michezo ikiendelea ndiyo tatizo.

Magari yaingie mapema, yazimwe, michezo iendelee. Sio mpira upo dakika ya 20, ndiyo mheshimiwa fulani anaingia uwanjani.

MADHARA YAKE

Moshi wa gari, hasa magari ya dizeli, ni hata ri kwa afya za binadamu kwa sababu husabanisha magonjwa ya ghafla na makali (acute conditions) au magonjwa ya muda mrefu kama saratani.

Ni bahati mbaya sana kwamba nchi yetu haiwekezi kwa kiasi kikubwa kwenye utafiti wa mambo kama haya.

Lakini utafiti uliofanywa mwaka 2013 na Chuo Kikuu cha Massachusetts Institute of Technology (MIT) cha Marekani inaonesha kwamba takribani vifo 53,000 hutokea nchini humo, kwa mwaka, kutokana na moshi wa magari!

Chuo hicho hicho kulifanya utafiti nchini Uingereza (UK) na kubaini kwamba takribani watu 5,000 hufariki kwa mwaka kutokana na moshi wa magari.

Hapa tunazungumzia Marekani na Uingereza ambako sheria za kutumia magari hasiruhusu magari yaliyotembea kilomita nyingi kutumika.

Vipi kuhusu sisi ambao tunatumia hadi magari ya miaka ya 1970?

Shirika la Afya duniani (WHO) kupitia wakala wake wa utafiti wa saratani (IARC), lilitoa matokeo ya utafiti wa mwaka 2015 na kusema moshi wa dizeli huongeza hatari ya saratani kwa wanaouvuta.

Kwanini tuwaweke wanamichezo wetu na hata watazamaji uwanjani katika hatari hii?

Acha tukutane na moshi mabarabarani huko kwa sababu hatuna namna, lakini viwanjani? Hapana...tuoneeni huruma jamani.

Hakuna haja wala ulazima wa magari kuingia viwanjani. Kwani katika vile viwanja ambavyo magari hayaingii, kitu gani hupungua?

Wakati umefika sasa kwa wasimamizi wa michezo na viwanja kulifikiria hili, la sivyo tutakuwa tunaendelea kuhatarisha maisha yetu wenyewe!

Asalaam Aleykum!