Madrid kupiga mnada mastaa kibao unaambiwa

Muktasari:

Kwa mujibu wa AS, mabosi wa timu hiyo wanahitaji kuchangisha walau Pauni 66 milioni kutoka kwenye wakazi itakaowauza ili kuongezea bajeti yao ya usajili.

MADRID, HISPANIA . REAL Madrid imekuja na mpango wa kupunguza bili yao ya mshahara kwa kuwaweka sokoni mastaa kibao kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi ili kuwapiga mnada.

Miamba hiyo ya Santiago Bernabeu inahusishwa na mastaa kibao wenye majina makubwa, lakini kunasa saini za wachezaji wapya ni lazima ipige bei kwanza kuchangisha pesa.

Kinachoelezwa ni kwamba Real Madrid inapiga hesabu za kuvuna pesa nyingi kwa kuuza wachezaji wanaoonekana kuwa ni nyongeza kwenye timu yao ili kupata pesa zitakazowafanya kuwa na nguvu kwenye kukamilisha dili wanazohitaji.

Kwa mujibu wa AS, mabosi wa timu hiyo wanahitaji kuchangisha walau Pauni 66 milioni kutoka kwenye wakazi itakaowauza ili kuongezea bajeti yao ya usajili.

Taarifa zinadai kwamba wachezaji ambao wanaweza kuingiza kwenye orodha ya watakaopigwa mnada ni Gareth Bale, James Rodriguez, Alvaro Odriozola, Mariano Diaz, Dani Ceballos na Jesus Vallejo, kwao hao wote watakapokuwapo sokoni dirisha litakapofunguliwa.

Kuachana na wachezaji sita kwa mara moja ni kitu kugumu kutokea, lakini mpango wa miamba hiyo ni kutafuta wateja wa mastaa wawili Bale na Rodriguez, hao ndio hasa inaotaka kuwaondoa kwenye kikosi ili kupunguza bili ya mishahara.