Mabao yaacha kilio, kicheko Ligi Kuu

Monday July 27 2020

 

By Charles Abel

WAKATI pazia la Ligi Kuu Bara 2019/20 likifungwa rasmi jana Jumapili, mabao yamegeuka lulu kwa kuamua hatima ya timu za kubaki kwenye ligi, kucheza hatua ya mchujo (play-off) na zile za kushuka daraja.

Tofauti na misimu mingine ambayo pointi ndizo zilikuwa zina nguvu katika kuamua hatima ya timu mbalimbali katika ligi, mambo yamekuwa tofauti msimu huu ambapo licha ya timu nne kulingana pointi, baadhi zimejikuta zikishuka daraja, kubaki kwenye ligi na kucheza mchujo licha ya kuwa na pointi sawa na nyingine.

Ushindi wa mabao 2-1 nyumbani dhidi ya Ruvu Shooting uliiokoa Mtibwa Sugar na kuiwezesha kubaki Ligi Kuu licha ya kulingana pointi na timu za Alliance, Mbeya City na Mbao.

Mtibwa Sugar ambayo baada ya ushindi huo imefikisha pointi 45, imebakia kwa kubebwa na utofauti mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa kulinganisha na wenzake ambapo imepachika mabao 30 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 34.

Timu nyingine iliyoweza kunusurika katika mechi ya mwisho ni Mwadui FC ambayo ushindi wake wa mabao 2-1 dhidi ya Kagera Sugar, umewafanya wafikishe pointi 47 ambazo zimewaacha salama.

Lakini haikuwa Mtibwa tu iliyookolewa na utofauti mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa kwani pia Mbao na Mbeya City licha ya kusota mkiani mwa msimamo wa ligi kwa muda mrefu, zimemaliza kwa ahueni angalau ya kucheza mechi za mchujo dhidi ya timu za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) baada ya kupata ushindi katika mechi zao.

Advertisement

Ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Ndanda katika mechi waliyocheza Uwanja wao wa nyumbani wa CCM Kirumba uliiwezesha Mbao kumaliza nafasi ya 16 kwenye msimamo wa ligi na hivyo kukata tiketi ya kucheza hatua ya mchujo.

Mbao ambayo ina pointi 45, imemaliza ikiwa imefunga mabao 33 na kufungwa 43 lakini nyingine iliyoponyeka ni Mbeya City ambayo baada ya kushinda mabao 3-0 dhidi ya KMC ugenini kwenye Uwanja wa Azam Complex imepata tiketi ya kucheza mchujo kwa kumaliza ikiwa imefunga mabao 33 na kufungwa 42.

Kocha wa Mbao, Felix Minziro amesema mshikamano, juhudi za wachezaji na makocha pamoja na sapoti ya viongozi na mashabiki ndio siri ya mafanikio yao.

"Tulikuwa kwenye hali mbaya lakini niliwajenga kisaikolojia wachezaji wangu katika hizi mechi za mwisho na kuwataka wapambane waweze kujiweka sokoni na wakafanya hivyo.

 

"Pia nawapongeza viongozi kwa kujitahidi kusaka chochote kitu cha kuwapa wachezaji na pia mashabiki kwa sapoti kubwa waliyotoa kwa timu," amesema Minziro

Lakini licha ya kujitutumua na kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Namungo FC kwenye Uwanja wa Nyamagana, Alliance iliangushwa na tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa na kujikuta ikishuka daraja licha ya kumaliza ikiwa pointi sawa na Mbeya City, Mtibwa na Mbao.

Alliance imemaliza nafasi ya 17 ikiwa imefumania nyavu mara 36 na yenyewe ikiruhusu mabao 48.

Kocha wa Alliance, Kessy Mziray amesema wamekubaliana na kilichotokea japo wamehuzunika na kilichotokea.

"Kilichotokea kimetokea. Tumepambana kuweza kutimiza malengo yetu lakini mwisho wa siku mambo hayajawa vizuri," amesema Mziray.

Lipuli ambayo ilikuwa inahitaji sare tu katika mechi yake dhidi ya Yanga ili icheze mchujo au ushindi ili ibaki moja kwa moja, ilishuka rasmi baada ya kuchapwa bao 1-0 kwenye Uwanja wake wa nyumbani wa Samora, bao lililopachikwa na David Molinga.

Ndanda, Alliance na Lipuli, zinaungana na Singida United ambayo ilitangulia kushuka daraja huku zikiwa zimebaki raundi saba kabla ya ligi hiyo kumalizika.

Kwingineko, Azam FC ilishindwa kumaliza nafasi ya pili na kuachwa kwenye mataa na Yanga, baada ya kulazimishwa sare ya mabao 2-2 ugenini dhidi ya Prisons.

Mabingwa Simba walimaliza vizuri kwa kuichapa Polisi Tanzania mabao 2-1 ugenini kwenye Uwanja wa Ushirika ambayo yalifungwa na nahodha wao John Bocco.

Coastal Union yenyewe ilifungwa bao 1-0 nyumbani na JKT Tanzania wakati Biashara United iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 ugenini mbele ya Singida United.

Advertisement