Mabao ya Yanga SC yako hapa

Tuesday September 15 2020

 

By Charles Abel na Oliver Albert

Dar es Salaam. Mabadiliko machache katika mbinu ya kiuchezaji na kimfumo yanaweza kuwa suluhisho la ubutu wa safu ya ushambuliaji ya Yanga katika kufunga mabao.

Ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mbeya City uliisaidia Yanga kupata pointi tatu, lakini bado kuna tatizo la ufungaji.

Mfumo wa kusimamisha mshambuliaji mmoja huku ikitegemea zaidi mashambulizi kutokea pembeni kwa mipira ya krosi limeifanya Yanga kuzipa urahisi timu pinzani katika kuwanyima nafasi.

Benchi la ufundi la Yanga, awali katika mchezo dhidi ya Prisons lilianza na mfumo wa 4-4-2, lakini katika mchezo uliofuata dhidi ya Mbeya City juzi Uwanja wa Benjamin Mkapa, lilitumia 4-3-3.

Michael Sarpong ambaye ndiye husimamishwa katika nafasi ya mshambuliaji pekee wa kati, hujikuta akizungukwa na kundi la walinzi wa timu pinzani ambao huwa rahisi kwao kuicheza na kuokoa mipira ya krosi.

Kwa bahati mbaya, Yanga imekuwa haishambulii kupitia katikati mara kwa mara, jambo ambalo huwa rahisi kutabirika kwa wapinzani.

Advertisement

Ukiondoa changamoto hiyo, sababu nyingine ambayo inaonekana kuikwaza Yanga ni baadhi ya nyota wake kutokuwa na uamuzi wa haraka au sahihi pindi wawapo na mpira na kujikuta wakiwanyima wenzao fursa muhimu za kufunga mabao.

Katika mechi mbili zilizopita dhidi ya Prisons na Mbeya City, winga Tuisila Kisinda na Yacouba Songne mara kadhaa walipata nafasi ambazo zingeweza kuwa fursa muhimu kwa timu kupata mabao wangeachia mpira haraka kwa wenzao.

Changamoto nyingine ambayo inaonekana inainyima fursa Yanga ya kupata idadi kubwa ya mabao ni kukosekana kwa wachezaji ambao wanaweza kuvunja ukuta wa timu pinzani hasa wanapokutana na timu inayojaza idadi kubwa ya wachezaji katika safu ya kiungo.

Tuisila Kisinda na Yacouba Songne ambao angalau wameonyesha wanamudu kuifanya kazi hiyo, mara kwa mara hucheza pembeni mwa uwanja ambako hutengeneza urahisi kwa wachezaji wa timu pinzani kuwadhibiti.

Beki wa zamani wa Yanga, Bakari Malima’ Jembe Ulaya’ alisema ni ngumu kuamini kwa sasa kuwa Yanga inaweza kupata mabao mengi katika mechi zake kwa sababu haina muunganiko mzuei.

“Wengi walikuwa wanahisi hivyo kwa Mbeya City sababu ya ilifungwa mabao 4-0 na KMC mechi iliyopita, lakini mambo yakawa tofauti.

“Hivi sasa Yanga inatengeneza timu na ubaya kocha alikuja kujiunga na kikosi hicho siku chache kabla ya kuanza ligi, hivyo bado yuko katika harakati za kutafuta muunganiko wa timu yake.

“Labda kuanzia mechi ya tisa au 10, hapo watu wataanza kuuona moto wa Yanga,” alisema Malima.

Kocha Mrage Kabange alisema: “Mbeya City ilivyocheza na KMC ni tofauti na ilivyocheza na Yanga, hivyo watu wanatakiwa kujua soka ndiyo liko hivyo, inatakiwa kumuheshimu mpinzani wako,” alisema Kabange.

Katika mchezo wa jana wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Namungo iliyokuwa nyumbani ilikubali kichapo cha bao 1-0 mbele ya Polisi Tanzania bao lililofungwa na Rashid Jumadakika ya 76.

 

Advertisement