Mabao nane yawastua Alliance FC

Muktasari:

Mzirai alisema kuna shida kwenye safu yake ya ulinzi ambayo imesababisha wafungwe mabao ya kizembe jambo ambalo wanatakiwa kulifanyia kazi.

ALLIANCE FC katika mechi tatu mfululizo walizocheza za Ligi Kuu wamefungwa mabao nane jambo ambalo limemstua kocha wao Kessy Mzirai ambaye amesema sasa ni lazima akomalie safu ya ulinzi kwani amegundua kuna shida kubwa eneo hilo.

Chama hilo lenye maskani yake eneo la Mahina jijini hapa, kufikia sasa wana alama 17 wakishika nafasi ya 11 katika msimamo wa Ligi Kuu Bara inayoongozwa na Simba wenye pointi 25.

Mzirai alisema kuna shida kwenye safu yake ya ulinzi ambayo imesababisha wafungwe mabao ya kizembe jambo ambalo wanatakiwa kulifanyia kazi.

“Tunafungwa mabao rahisi sana. Mabeki wanashindwa kuzuia mianya ya mipira ambayo ndio inayofanya wapinzani wetu watufunge, kitu ambacho tunatakiwa kukifanyia kazi kwa sasa,” alisema Mzirai.

Alisema walifanyia kazi tatizo hilo baada ya kufungwa mabao 5-0 na Azam FC lakini bado udhaifu ulijirudia walipocheza dhidi ya Yanga na kufungwa bao 2 -1 katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini hapa.

“Tulifanyia kazi hili tatizo baada ya mchezo wetu na Azam lakini ikajirudia tena. Angalia katika mchezo na Yanga yale makosa mawili ya kushindwa kukaba ndio yalitugharimu na kupoteza mchezo,” alisema.

Hata hivyo, kocha huyo alisema ligi ni ngumu hivyo wataendelea kupambana katika mechi sijazo ambapo amewataka mashabiki waendelee kuwapa sapoti huku wao benchi la ufundi wakiweka sawa kasoro zilizojitokeza.