Mabao 1,072 yafungwa waafrika wagawana kiatu cha dhahabu Ligi Kuu England

Muktasari:

Misimu iliyofuatia baada ya hapo, imeshindwa kuleta mabao mengi hadi huu uliomalizika juzi, ambapo nyavu zilitikisika mara 1,072.

LONDON, ENGLAND. AFRIKA imeweka nembo yake kwenye Ligi Kuu England. Mastaa watatu waliofunga mabao mengi kwenye ligi hiyo msimu uliomalizika juzi Jumapili, wote wanatoka kwenye Bara la Afrika.

Sadio Mane wa Senegal, Mohamed Salah wa Misri na Pierre-Emerick Aubameyang wa Gabon. Wakali hao kila mmoja amefunga mabao 22 na hivyo kugawana tuzo ya mfungaji bora kwenye Ligi Kuu England, kila mmoja akikabidhiwa Kiatu cha Dhahabu.

Lakini, unaambiwa hivi, msimu huu wa Ligi Kuu England umeshuhudia mabao mengi sana yakifungwa kuliko misimu mingine yote iliyopita.

Vita ya ubingwa ilikuwa ya timu mbili, Manchester City na Liverpool, lakini vita ya kusaka Kiatu cha Dhahabu iliwahusisha mastaa wengi na ndio maana supastaa wa Arsenal, Aubameyang ni mmoj ya walionyakua kiatu hicho.

Hii ni mara ya kwanza kushuhudia mabao mengi hivyo yakifungwa ndani ya msimu mmoja tangu mwaka 1992. Huko nyuma, msimu ambao ulishuhudia mabao mengi ya yakifungwa ulikuwa ule wa 2011-12, ambapo mabao 1,066 yaliwekwa nyavuni.

Misimu iliyofuatia baada ya hapo, imeshindwa kuleta mabao mengi hadi huu uliomalizika juzi, ambapo nyavu zilitikisika mara 1,072.

Christian Eriksen alivunja rekodi kwa kufunga bao la 1,067, wakati Mark Noble alifunga bao la 1,068, Andros Townsend bao la 1,069, Sadio Mane bao la 1,070, Salomon Rondon bao la 1,071 na Eddie Nketiah wa Arsenal ndiye aliyepiga bao la mwisho kabisa la msimu, ambapo ni la 1,072.

Mabao mengi yote hayo, hakuna mchezaji mmoja aliyefunga mara nyingi kuliko wenzake. Hakuna pia aliyezidi mabao 22 baada ya mastaa hao watatu, Mo Salah na Mane wa Liverpool na yule wa Arsenal, Aubameyang kufunga mara 22 na kugawana Kiatu cha Dhahabu. Hii ilikuwa kama mwaka 2011, ambapo Carlos Tevez akiwa Man City na Dimitar Berbatov wa Manchester United waligawana tuzo hiyo ya ufungaji bora baada ya kila mmoja kufunga mabao 20.