MTAA WA KATI : EPL inarudi na tishio la Newcastle United

Wednesday June 12 2019

 

By Said Pendeza

ALHAMISI wiki hii ratiba ya Ligi Kuu England kwa msimu wa 2019/20 itapangwa. Hiyo itakuwa ni ratiba ya awali ambayo itasubiri mambo ya televisheni ili kuzipangia siku na tarehe za kufanyika mechi zake.

Lakini, kubwa timu zitafahamu mapema ligi inaanza lini na ni mpinzani gani atakayeanza naye, nyumbani au ugenini.

Ni vyema kulifahamu hilo mapema. Lakini, hapo kwenye ratiba ndipo panaponifanya nifikirie kuhusu Top Four itakavyokuwa msimu ujao.

Msimu huu, vigogo wawili Arsenal na Manchester United waliachwa nje, hivyo hawatakuwa kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Top Four ilikuwa na Manchester City, Liverpool, Chelsea na Tottenham Hotspur. Msimu ujao itarudi kwa mtazamo upi?

Ni swali linalohitaji subira kupata majibu yake. Kocha Ole Gunnar Solskjaer atakuwa na muda wa kutosha kuiandaa timu yake ya Man United walau msimu ujao kupambana kuwamo kwenye Top Four.

Advertisement

Unai Emery huo utakuwa msimu wake wa pili, hivyo hatakuwa mgeni tena na upinzani uliopo kwenye ligi hiyo, hivyo atapambana kuhakikisha Arsenal inarejea kwenye timu nne za juu na kukamatia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kushindwa kufanya hivyo kwa misimu mitatu mfululizo.

Jurgen Klopp huko Liverpool na Pep Guardiola Man City, wao vita yao itaendelea kubaki kwenye kufukuzia ubingwa na si kufikiria kuwamo kwenye Top Four.

Spurs watakuwa na nguvu pia kama mastaa wake wataendelea kubaki na Mauricio Pochettino atapewa pesa za kusajili, wakati Chelsea bado kuna maswali mengi, Eden Hazard ameondoka na timu imefungiwa kusajili, huku kocha wao Maurizio Sarri akihusishwa na mpango wa kuondoka kwenye timu hiyo kwenda Juventus. Vita ni kubwa.

Lakini, wakati vita hiyo yenyewe ikiwa kubwa. Kuna wasiwasi mpya unakuja kuhusu Newcastle United.

Klabu hiyo si muda mrefu inaweza kuwa chini ya bilionea wa Kiarabu, Sheikh Khaled bin Zayed Al Nehayan.

Hilo likitokea, basi Newcastle inakuwa na pesa nyingi za kufanya usajili wa wachezaji inaowahitaji. Mpango wa Newcastle pia ni kumchukua Jose Mourinho kuwa kocha wao mpya.

Hakuna asiyefahamu vurugu za Mourinho anapokuwa kwenye timu yenye pesa ya kusajili. Bila ya shaka ataleta mastaa wa maana na kuifanya St James Park kuwa mahali pagumu kwenye kuchukua pointi kizembe.

Kama hilo likitokea, Newcastle wakasajili mchezaji wanayemtaka, wakawa chini ya Mourinho, bila ya shaka pale kwenye Top Four patakuwa na mtikisiko mkubwa.

Hakutakuwa na habari za Big Six tena, kutakuwa na Big Seven na pengine kuna vigogo hapo watakuwa kwenye hali mbaya zaidi.

Sawa, bilionea huyo wa Kiarabu atahitaji kufanya mambo mengi zaidi kuifanya Newcastle kuwa timu tishio, lakini kutoa pesa ya kusajili na kisha akakabidhiwa kocha mwenye mipango ya ushindi kama Mourinho, bila ya shaka kuna jambo tofauti linaweza kutokea kwenye ligi hiyo kwa msimu ujao. Hiki ndicho ninachosubiri kukiona.

Advertisement