MDAMU : Mkali wa Ndondo aliyeitibulia Simba

Muktasari:

Straika huyo chipukizi anazungumza na Mwanaspoti akieleza maisha yake alipotoka ,alipo, mikakati na malengo yake kwenye kazi yake ya mpira.

HABARI ya mjini kwa sasaNYOTA wa Mwadui FC, Gerard Mathias kwa sasa ndiye habari ya mjini kutokana na kazi nzuri aliyoifanya juzi kwa kuvunja rekodi ya Simba ambao walikuwa hawajaonja kichapo kwenye Ligi Kuu.

Kinda huyu ambaye alikuwa hapati nafasi kwenye kikosi cha Mwadui, ameibuka msimu huu chini ya Kocha Khalid Adam na kufanya mambo makubwa na kuwa kipenzi cha mashabiki mjini Shinyanga.

Mathias ambaye kwa sasa ameisaidia Mwadui kuwa na pointi 10 ameifungia mabao manne na kuingia kwenye orodha ya wachezaji wenye mabao mengi akitanguliwa na nyota wa Simba, Meddie Kagere mwenye saba.

Straika huyo chipukizi anazungumza na Mwanaspoti akieleza maisha yake alipotoka ,alipo, mikakati na malengo yake kwenye kazi yake ya mpira.

Historia yake

Mathias anasema mwaka 2016 ndio aliibuliwa na Mwadui FC akiwa kwenye michuano ya Ndondo Cup akikipiga timu ya Tabata United,ambao walikubali uwezo wake.

Anasema timu hiyo ilimchukua kwa sharti moja tu,kuwa atawekwa timu ya vijana na akikomaa atapandishwa katika kikosi cha wakubwa jambo ambalo hakulipinga.

Anasema kwa kipindi ambacho alikuwa katika timu ya vijana akawa anaonyesha uwezo, jambo ambalo lilimvutia aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ kuanza kusafiri naye kwa baadhi ya mechi za kirafiki.

Anasema katika moja ya mechi ambayo ilimpa ulaji ilikuwa mkoani Tabora ikiwa ya kirafiki,ambapo wachezaji viungo (Namba sita) waliumia wote na Julio kuuliza kama kuna anayeweza kusaidia.

“Julio alikuja kwenye benchi nani anaweza kuingia namba sita akamalizia hizi dakika, akaniuliza kama ninaweza nikamwambia sijawahi kucheza nafasi hiyo ila ngoja niingie nijaribu,” anasema nyota huyo.

“Kuanzia hapo Julio akaanza kunipa namba kwenye timu ya wakubwa na mechi ya kwanza ilikuwa dhidi ya Kagera Sugar tulifungwa bao 1-0,lakini hata mabosi wa Kagera Sugar wakanihitaji sikutaka kwenda haraka,” anasema.

Anasema baada ya Julio kuondoka na kuingia Ally Bushiri ‘Benitez’ akawa hampi namba kwa kutokubali uwezo wangu hadi msimu ulipoisha kabla ya kuja kwa Jumanne Ntambi (Marehemu).

Anasema Kocha Ntambi alianza kumtumia lakini Kagera Sugar wakiendelea kusaka saini yake,ambapo kipindi hicho Kocha Khalid Adam aliweza kuungana na Mwadui.

Anasema ujio wa Kocha huyo uliibua matumaini kwake kutokana na kumuamini kumpanga kikosini na alipoondoka Mwadui kujiunga na Ndanda yeye alibaki kikosini.

Anasema Adam alipoondoka na nafasi yake kuchukuliwa na Ally Bizimungu,bado nafasi yake kikosini ilizidi kuwa finyu, hadi msimu huu aliporejea Adam ambaye amempa nafasi ya kila mechi.

“Kwahiyo sikukata tamaa kwa mabadiliko hayo,isipokuwa nilikuwa najaribu kuonyesha uwezo kwa kila nilipopata nafasi lakini Makocha wana mtazamo wao kwa mchezaji na mechi husika,” anasema Mathias.

Malengo yake

Kinda huyu anasema kuwa moja ya malengo yake ni kupambania nafasi kikosini kutokana na vita ya ushindani wa namba kuwa mkali ili kuendeleza kipaji chake.

Anasema mbali na hilo, anapambana kwa uwezo wake kuweza kuisadia timu hiyo kukwepa rungu la kukwepa kushuka Daraja na kutocheza Ligi ya mchujo ‘Play Off’.

Anasema msimu uliopita walipitia kipindi kigumu hadi kuponea dakika za mwisho kushuka daraja, hivyo msimu huu hawataki yawakute tena na ndio maana kila mmoja anapambana.

Pia anaeleza kuwa malengo yake ni kucheza soka la kulipwa nje ya nchi kama wachezaji wengine wanaofanya vizuri na kuitanga za Tanzania katika medani za Soka ulimwenguni.

“Taifa Stars naiwaza sana lakini ninaamini siku ikifika nitaitwa na nitafanya kazi nzuri ili kuitumikia Taifa langu, natamani kucheza soka la kulipwa nje ya nchi kama wengine wanavyofanya,” anasema Mathias.

Kuhusu Simba na Yanga

Kinda huyu anasema kwanza anafurahi kuifunga Simba na kwamba zipo nyingine aambazo ameshazifunga,hivyo kumfanya kufikia moja ya ndoto zake kuzifunga Klabu kubwa hapa nchini.

Anasema ikitokea timu za Simba na Yanga kuhitaji huduma yake,yeye hana tatizo,kwani hatua ya kujiunga na vigogo hao ni moja ya safari zake kwenda mbali zaidi.

Anasema iwapo atapata namba katika moja ya timu hizo hatasita kujiunga nayo na itaweza kusaidia kufikia ndoto zake,huku akiweka wazi kuwa hafikirii kuwekwa benchi na mchezaji yeyote.

“Napenda kucheza katika timu za Simba na Yanga ili kuwa moja ya ngazi kupandia kwenda mbali haswa kwenye soka la kulipwa nje ya nchi, kwahiyo ikitokea wakanihitaji niko tayari kufanya kazi,” anasema Mathias.

Chipukizi huyo anaongeza kwamba mbali na Simba na Yanga,lakini pia Azam ni moja ya timu zinazomuumiza akili kutamani kuzitumikia ili kufikia malengo.

Kagere amchanganya

Straika huyu mwenye mabao manne kwa sasa,anasema licha ya ushindani uliopo katika vita ya ufungaji mabao,lakini anapambana kuhakikisha anakula sahani moja na nyota wa Simba,Meddie Kagere.

Anasema kuwa Kagere amekuwa na kasi kubwa na ni mpambanaji ambaye muda wote anafikiria kufunga, jambo ambalo linamfanya kujiandaa zaidi na kimbinu ili kukabiliana naye.

Anaeleza kuwa anatamani zaidi kufikia mafanikio ya mtangulizi wake, Salim Aiyee kwa kile alichokifanya ndani ya Mwadui FC na pengine kumpita,hivyo ataendelea kupambana kadri ya uwezo wake.

“Natamani sana kuwa mfungaji bora,naelewa ushindani uliopo haswa kwa Kagere ambaye muda wote anafikiria kufunga,kwahiyo nitaendelea kupambana kama walivyofanya Aiyee na wengine”anasema Straika huyo.

Amtaja Nyoni

Mshambuliaji huyu ambaye aliipenya ngome ya Simba juzi na kufunga bao pekee lililoihakikishia Mwadui pointi tatu,anasema moja ya beki bora hadi sasa ni Erasto Nyoni.

Anasema licha ya kwamba alitumia akili na mbinu nyingi kuwafunga Simba katika mazingira magumu,lakini Nyoni alimpa wakati mgumu na hawezi kumsahau.

Anasema beki huyo alionekana kumbana muda wote haswa baada ya kutupia bao na kumfanya uwanjani kuonekana kama anacheza peke yake.

“Moja ya beki katili niliyeona mkali sana kwangu hadi sasa ni Nyoni,jamaa anakaba sana tena kwa nguvu licha ya kwamba niliwafunga ila nilikutana na ushindani mkali,” anasema.

Anaongeza kuwa mbali na Nyoni,beki mwingine ni Idd Moby wa JKT Tanzania ambaye alimsumbua wakati wa mechi yao iliyomalizika kwa sare ya mabao 2-2.

Pia Mchezaji huyo anasema mbali na mabeki,timu bora kwake kwa mechi walizocheza kwa sasa ni JKT Tanzania ambayo iliwapa ushindani katika mechi yao.

“JKT Tanzania ndio naona timu bora hadi sasa,kwa sababu tuliwatangulia kufunga mabao mawili lakini walipambana na kusawazisha na kama ingetokea dakika tungefungwa pale nyumbani,” anasema mkali huyo.