Lwandamina apata mrithi wa Ngoma

Saturday January 13 2018

 

By KHATIMU NAHEKA

YANGA imewapa nyota wake mapumziko ya siku mbili hadi kesho Jumapili kabla ya kuanza kujifua na mechi yao ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Mwadui, lakini habari njema kwa mashabiki wake ni kwamba, mrithi wa Donald Ngoma amepatikana.

Ngoma na Amissi Tambwe wamekosekana kwa muda mrefu ndani ya kikosi cha Yanga kutokana na kuwa majeruhi na kuwapa presha Wana Jangwani, lakini kocha George Lwandamina ametumia dakika 90 kugundua kitu kwa straika mpya chipukizi Yohana Mkomola na kutamka; “Huyu akitulia anakinisikiliza atakuwa Ngoma mpya.”

Mkomola aliyesajiliwa na Yanga kwenye dirisha dogo akitokea kikosi cha Timu ya Taifa ya Vijana U17, amemkuna mno Mzambia huyo na kudai kama akituliza akili akawasikiliza makocha wake atakuwa ni mwiba mkali uwanjani.

Akizungumza na Mwanaspoti, Lwandamina aliyeamua kukaa jukwaani katika mchezo wa mwisho kati ya Yanga dhidi ya URA na timu yake kung’olewa michuano ya Mapinduzi kwa matuta, aligundua kuwa Mkomola ni moja ya kipaji bora walichonacho katika safu yao ya ushambuliaji.

Alisema Mkomola ni moja kati ya usajili bora waliowahi kuufanya ambapo, kama ataendelea kuwa msikivu na kudumisha nidhamu atakuwa na bonge la mchezaji katika kikosi hicho kwenye michezo ya Ligi Kuu na hata kimataifa.

Alisema kinda huyo anaonekana kuwa na makali ikiwemo kasi akiwa pia na ubora wa kujua kujitenga katika maeneo mazuri ya kufunga, lakini anahitaji kuongezewa vitu vichache tu. “Angalia akitoa pasi anachofanya hazubai anakimbilia sehemu sahihi kusubiri afunge, pia anapenda kuhakikisha kama hapa kipa kashadaka au nafasi imepotea ni moja kati ya vipaji bora tumevipata,” alisema Lwandamina.

“Ukiwa kocha sio kila wakati utapata mchezaji aliyekamilika kuna vitu vimepungua kwake nitapambana kumbadilisha taratibu, lakini naamini kama akiwa msikivu na akidumisha nidhamu nitamfanya kuwa mchezaji bora katika safu ya ushambuliaji.

“Uwezo wake ni kama alionao Ngoma, ambaye kwa muda mrefu amekuwa nje ya uwanja, ila Mkomola akikaa sawa atafukia mashimo yote ya safu ya ushambuliaji.”