Lusajo hatihati kuivaa Simba

Wednesday July 29 2020

 

By Yohana Challe

KOCHA Mkuu wa Namungo FC, Hitimana Thierry amesema mshambuliaji wake, Reliants Lusajo huenda akaukosa mchezo wa fainali dhidi ya Simba.

Hitimana amezungumza na Mwanaspoti Online kwa njia ya simu leo Jumatano, Julai 29, 2020 kutoka Sumbawanga kuwa licha ya kusafiri na mchezaji huyo kwenye mechi ya fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) itakayochezwa Agosti 2, 2020 lakini ana asilimia chache za kucheza.

"Nimesafiri na wachezaji wote 26 kwa ajili ya kuvaa medali, lakini wale waliokuwa majeruhi katika michezo ya mwisho ya ligi wanaendelea vizuri.

"Bigirimana (Blaise) anaweza akacheza lakini Lusajo hali yake haijakuwa nzuri japo naye yupo huku," amesema Hitimana.

Namungo imewasili Sumbawanga tangu jana Jumanne na leo jioni Jumatano inatarajia kufanya mazoezi kujiandaa na mchezo huo utakaochezwa Jumapili Uwanja wa Nelson Mandela, Sumbawanga.

Lusajo amemaliza kinara wa mabao kwenye kikosi hicho akiwa amefumania nyavu mara 12.

Advertisement

Namungo iliyomaliza nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na alama 64 na kutinga hatua ya fainali ya ASFC imejikatia tiketi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika.

Advertisement