Luhende awaza kuiliza Simba

Saturday September 21 2019

 

By OLIPA ASSA

BEKI wa Kagera Sugar, David Luhende ameuzungumzia mchezo wao na Simba utakaopigwa Septemba 26 mwaka huu kwamba utakuwa mgumu lakini anaamini wataendeleza rekodi ya ushindi.
Msimu ulioisha Simba ilipigwa na Kagera Sugar nyumbani na ugenini, jambo linalowafanya nyota wao kutamba kuendeleza kichapo hicho.
Luhende amesema licha ya kuamini kushinda mchezo huo, wanawaheshimu Simba kuwa na wachezaji wenye uwezo wa hali ya juu ambao watafanya mchezo uwe mgumu na ushindani wa juu.
"Ni kweli tuliwashinda Simba nyumbani na ugenini, hii haina maana kwamba ni wabaya bali ni matokeo ambayo yanaamuliwa na dakika 90, hivyo tutaingia kwa kupambana"
"Hakuna kitu kizuri kucheza na timu ambayo unaijua ubora na udhaifu wake, unakuwa unajua ufanye nini ili kupata matokeo, ingawa hata Simba wataingia kwa kupambana ili kufuta rekodi ya kuwafunga kila mara"amesema.
Simba inasafiri kuifuta Kagera Sugar na kocha wao Patrick Aussems amekiri utakuwa mchezo mgumu amekiri hajaishinda timu hiyo.
"Si mechi rahisi ikumbukwe sijaifunga Kagera Sugar, maandalizi yangu yalikuwa ya mbinu zaidi, naamini awamu hii kitaeleweka"amesema.

Advertisement