Staa wa zamani Liverpool asema hashangai sadio kutakiwa na Real Madrid

Muktasari:

Kwa msimu uliopita, Mane alikuwa muhimu wakati Liverpool ilipokwenda kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kuwachapa Tottenham Hotspur katika mchezo wa fainali uliopigwa huko Wanda Metropolitano, Madrid, Hispania.

LIVERPOOL, ENGLAND . STAA wa zamani wa Liverpool, Jamie Redknapp amemtazama Sadio Mane anachokifanya huko Anfield na kusema: “Huyu jamaa ni mashine.”

Kiwango cha fowadi huyo Msenegali anachokionyesha kwenye kikosi hicho kinachonolewa na Jurgen Klopp ni bora kwelikweli akiisaidia kubeba Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita huku wakishindwa kidogo tu kubeba taji la Ligi Kuu England, lakini akiwasogeza kwenye hatua nzuri ya kunyakua ubingwa huo msimu huu.

Redknapp alisema kwa muda wa miezi 18, Mane amekuwa kwenye kiwango bora na jambo hilo ndilo linalozifanya klabu mbalimbali Ulaya wakiwamo Real Madrid kuhitaji saini yake. Ubora wa soka lake ulimfanya ashike namba nne kwenye tuzo za Ballon D’Or huku akipigiwa kura na supastaa wa dunia, Lionel Messi.

Kwa msimu uliopita, Mane alikuwa muhimu wakati Liverpool ilipokwenda kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kuwachapa Tottenham Hotspur katika mchezo wa fainali uliopigwa huko Wanda Metropolitano, Madrid, Hispania.

Tangu wakati huo Real Madrid wamekuwa wakifukuzia saini yake na huenda kila kitu kuhusu uhamisho wake kikafanyika kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi.

Kwenye hilo la kutakiwa na Real Madrid na wakati mwingine akihusishwa na Barcelona, Redknapp alisema wala hawezi kushangaa kwa sababu mchezaji wa aina yake ni kawaida kuhusishwa na timu zote kubwa duniani.

“Aliposajiliwa na Liverpool kutokea Southampton wengi tulishtuka, lakini tangu hapo amekuwa kwenye kiwango bora sana.

“Amekuwa moto kwelikweli. Ana nguvu, mzuri hewani, anashambulia na anapiga miguu yote.

“Ni mchezaji wa aina yake, mzuri sana kwenye kuwafanyia ujanja mabeki asiotee na amekuwa akiunganisha wenzake kwenye fowadi, akiwamo mshambuliaji wa kati Roberto Firmino.

“Ukweli ni kwamba amekuwa kama mashine katika kila mechi. Amekuwa akifunga mabao, tena mabao makali na wala hajali na hilo ndilo linalomfanya kuwa kwenye daraja la peke yake.”

Msimu uliopita, Mane alikuwa mmoja wa wachezaji waliobeba Kiatu cha Dhahabu kwenye Ligi Kuu England, baada ya kufunga mabao sawa na staa mwenzake wa Liverpool, Mo Salah na supastaa wa Arsenal, Pierre-Emerick Aubameyang. Wakali hao wote kutoka Afrika kila mmoja alifunga mabao 22 wakati walipogawana tuzo hiyo ya ufungaji bora kwenye Ligi Kuu England.

Msimu huu, Mane ameachwa nyuma kwa mabao na fowadi mwenzake wa Liverpool, Mo Salah, lakini kuhusu mchango wake wa kuisaidia timu hiyo ya kocha Jurgen Klopp hauna mjadala.

Kiungo wa zamani wa Liverpool na Real Madrid, Steve McManaman alisema kwamba haoni kama Mane atakwenda kujiunga na Los Blancos na kinachotokea kwa sasa ni uvumi tu.

“Nitazichukua hizi kama tetesi tu kwamba Real Madrid wanamtaka Sadio Mane. Lakini, hapo kuna chumvi inawekwa,” alisema.

“Sidhani kama kuna jambo kama hilo la ama Mane au Mohammed Salah kwenda kujiunga na Real Madrid au Barcelona.”

Kwa muda mrefu mastaa hao wa Anfield wamekuwa wakihusishwa na miamba hiyo ya soka ya Hispania huku wengi wakitega masikio na kusubiri kwa hamu kuona kama kuna dili lolote litakalowahusu litakalofanyika kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi.