Lipuli waanza maandalizi kivivu

Wednesday June 3 2020

 

By OLIVER ALBERT

KOCHA wa Lipuli Nzeyimana Mailo amesema  wachezaji wake wote hawako fiti na wameonyesha kuwa hawakuwa wakifanya mazoezi binafsi kipindi ligi ikiwa imesimama hivyo ana kazi ya ziada kuweza kurejesha ubora wa kikosi hicho kabla ya ligi kurejea.

Ligi Kuu Bara imepangwa kurejea Juni 13 baada ya kusimama kwa miezi miwili kutokana na mlipuko wa virusi vinavyosababisha ugonjwa wa covid19.

Wakati ligi iliposimama  wachezaji wa timu mbalimbali walikuwa wakifanya mazoezi binafsi majumbani mwao huku wakifuata programu za makocha wao, lakini kocha Nzeyimana anaona kwa timu yake imekuwa tofauti.

Nzeyimana alisema kwa jinsi alivyowaona wachezaji wake mazoezini wanaonyesha wazi kwamba hawakufanya mazoezi binafsi hivyo itamlazimu kuendelea na programu ya mazoezi mara mbili kwa siku ili kuwaweka fiti kabla ya ligi.

"Ninachoshukuru asilimia kubwa ya wachezaji wamejiunga na timu na tunaendelea na mazoezi hivyo hata ligi ikianza sina wasiwasi kwani wachezaji wapo.

"Kikubwa nilichokiona kwao wengi hawako fiti na inaonekana hawakuwa wakifanya mazoezi kabisa hivyo, lazima tupambane siku zilizobaki kufanya mazoezi ya nguvu ili timu iweze kuwa fiti.

Advertisement

"Tutafanya mazoezi mara mbili kwa siku na tutaangalia mwishoni mwa wiki tunaweza kutafuta mechi ya kirafiki ili izidi kutupa uimara zaidi," alisema Nzeyimana.

Lipuli itacheza na Polisi Tanzania Juni 20 katika mchezo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Ushirika Moshi.


Advertisement