Ligi kuchezwa Dar kizungumkuti

Saturday May 23 2020

 

By Waandishi Wetu

HADI  muda huu leo Jumamosi jioni hakijaeleweka juu ya  Ligi Kuu kupigwa  katika kituo kimoja  jijini Dar es Salaam, licha ya Waziri wa Michezo, Dk Harrison Mwakyembe kutangaza hivyo  jana Ijumaa .

Leo Jumamosi asubuhi vigogo wa Bodi ya Ligi na wale wa Serikali pamoja na Shirikisho la Soka nchini (TFF) wamekutana ili kuweka mambo sawa kabla ya Ligi kuendelea baada ya Rais Dk.  John Pombe Magufuli kuruhusu michezo ianze Juni Mosi.

Hadi saa 12 jioni kikao hicho kilikuwa kinaendelea huku ikielezwa kuwa utata huko kwenye mkoa gani Ligi Kuu ichezwe, licha ya Waziri Mwakyembe kueleza itachezwa Dar es Salaam.

Alisema ili kuchukua tahadhari ya janga la corona, ligi kuu itachezwa kwenye viwanja vya Taifa, Uhuru na Chamazi vyote vya Dar es Salaam, tofauti na utaratibu wa awali wa mechi za nyumbani na ugenini.

Alisema mechi za FA pia zitachezwa Dar es Salaam huku zile za Ligi daraja la kwanza na la pili zikichezwa jijini Mwanza.

Hata hivyo leo ajenda hiyo ilichukua nafasi kubwa kwenye kikao hicho  kilichofanyika Dar es Salaam, licha ya kujadili pia mambo mengine yatakayojiri mara Ligi itakaporejea.

Advertisement

Habari za ndani ya kikao hicho zimeidokeza MCL Digital kuwa licha ya Waziri kueleza Ligi kuchezwa Dar es Salaam, Bodi nao walitaka ligi ichezwe kituo kimoja lakini  nje ya Dar es Salaam kwa kukubaliana na klabu.

"Walitaka wakubaliane kwanza na klabu waone ni wapi itafaa, hivyo Waziri alitangaza itachezwa Dar es Salaam bila kuishirikisha Bodi,".

"Wengi hawakubaliani na hilo na ndilo limetumia muda mrefu kujadiliwa mpaka sasa kikao hakijakwisha," alisema mmoja wa wajumbe wa kikao hicho ambaye aliomba hifadhi ya jina.

 

Advertisement