Ligi Kuu England ilivyotengeneza maswahiba kibao

Muktasari:

  • Hii hapa ndio orodha ya maswahiba wakubwa waliopo kwenye Ligi Kuu England kwa sasa.

LONDON, ENGLAND .LIGI Kuu England ni mahali ambako wachezaji wa karibu dunia nzima wametua na kucheza soka kwenye ligi hiyo.

Lakini wachezaji hao wanaotoka pande mbalimbali za dunia, baadhi wamejikuta wakitengeneza urafiki unaokaribia kuwa undugu kwa maana ya kusaidiana ndani na nje ya uwanja. Kwa miaka mingi huko kwenye Ligi Kuu England kumeshuhudiwa maswahiba kibao, kuanzia Dwight Yorke na Andy Cole, David Beckham na Gary Neville, Frank Lampard na John Terry na wengine kibao.

Hii hapa ndio orodha ya maswahiba wakubwa waliopo kwenye Ligi Kuu England kwa sasa.

Salah na Dejan Lovren

Utashangaa lakini huko Liverpool straika Mohamed Salah swahiba wake mkubwa ni beki wa kati, Dejan Lovren. Ungeweza kufikiria Mo Salah angetengeneza urafiki mzuri kabisa na wale wachezaji wenzake kwenye safu ya ushambuliaji, Roberto Firmino na Sadio Mane, lakini staa huyo wa kimataifa wa Misri, swahiba wake ni Lovren.

Lovren ndiye aliyekuwa akimwelekeza njia za kupita Mo Salah wakati alipotua huko Anfield na tangu hapo wamekuwa maswahiba wakubwa kwenye kikosi hicho kinachonolewa na Mjerumani, Jurgen Klopp.

Alexandre Lacazette na Pierre-Emerick Aubameyang

Tangu alipokwenda kuungana na Alexandre Lacazette huko Arsenal kwenye dirisha la Januari mwaka jana, straika Pierre-Emerick Aubameyang amekwenda kutengeneza uswahiba matata kabisa huko Emirates. Wawili hao wamekuwa na urafiki kiasi cha kwamba hata mmoja anapofunga bao uwanjani, wamekuwa wakishangilia pamoja na kuanzisha staili yao binafsi ya ushangiliaji.

Lacazette amekiri wazi anamchukulia Aubameyang kama ni kaka yake na anadai anafurahia sana kuona wanafanya kazi pamoja kwenye kikosi hicho cha Arsenal.

Romelu Lukaku na Paul Pogba

Wakati wa Jose Mourinho, Manchester United kulikuwa na shida kubwa kwelikweli baina ya wachezaji, lakini hilo halikuwatikisa maswahiba wawili, Romelu Lukaku na Paul Pogba.

Huko nyuma, Jesse Lingard alitengeneza urafiki na Pogba, lakini urafiki huo hauwezi kupita ule wa Pogba na Lukaku.

Wawili hao wamekuwa na urafiki wa karibu sana na hata uamuzi wa Lukaku kuhamia Man United unadaiwa ulichangiwa sana na Pogba. Kumbuka Mourinho aliwahi kutibuana na Lukaku walipokuwa Chelsea na wakati anamtaka, Chelsea nao walikuwa wakimtaka, lakini kwa muda huo, Pogba alikuwa karibu na Lukaku huko Marekani kwenye mapumziko ya mwishoni mwa msimu na hapo Man United ikafanikiwa kumnasa. Wawili hao urafiki wao unatambulika kwa jina la ‘Pogkaku’.

Dele Alli na Eric Dier

Huko kwenye kikosi cha Tottenham Hotspur, kuna maswahiba wawili, Dele Alli na Eric Dier.

Dele na Dier wamekuwa hata wakikaa chumba kimoja kwenye hoteli pindi Tottenham inapokuwa kwenye mechi za ugenini na hata kwenye manunuzi yao ya bidhaa mbalimbali wamekuwa wakitoka pamoja. Wawili hao wamekuwa wakipeana sapoti kubwa sana, wakipongezana pindi mmoja wao anapofunga bao. Dele aliingilia kati ugomvi baina ya swahiba wake Dier na mchezaji mwenzao kwenye kikosi cha Spurs, Danny Rose.

Richarlison na Yerry Mina

Huu ni ushkaji unadaiwa ni wa mwendokasi. Mastaa hao wawili wote ni wapya huko Everton. Wachezaji Richarlison na Yerry Mina ni marafiki wa karibu sana huko kwenye kikosi cha Goodison Park. Mara kadhaa wamekuwa wakionekana pamoja kwa migawaha na maduka mbalimbali huko jijini Liverpool. Picha zao nyingi walizopiga pamoja wamekuwa wakiziposti kwenye kurasa zao za Instagram. Richarlison na Mina walinaswa na Everton kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi mwaka jana.

Benjamin Mendy na Bernardo Silva

Kwa sasa Benjamin Mendy na Bernardo Silva wanakipiga kwenye kikosi cha Manchester City, lakini wawili hao walikuwa pamoja pia AS Monaco. Ilikuwa rahisi sana kwa Man City kuwapata wachezaji hao kwenye kikosi chao baada ya kumchukua mchezaji mmoja. Bernardo Silva hata wakati mwingine anapofunga, amekuwa na kawaida ya kwenda kushangilia na Mendy. Kisha Mendy aliandika kwenye Twitter kwamba anampenda sana Silva kuliko hata mpenzi wake.