Lewandowski na mastaa wengine wa timu moja waliopigana wenyewe

Saturday April 13 2019

 

MUNICH, UJERUMANI

SUPASTAA wa Bayern Munich, Robert Lewandowski ameripotiwa kupigana ngumi na mchezaji mwenzake, Kingsley Coman.

Wachezaji hao wawili waliwashangaza wenzao huko mazoezini baada ya kurushiana makonde ya haja na kuumizana usoni. Kinachoelezwa ni kwambaa Lewandowski alisema kitu mbele ya Coman ambacho hakikumfurahisha Mfaransa huyo. Wawili hao waliona kujibizana kwa maneno haitoshi, wakaamua kurushiana makonde.

Wawili hao wameripotiwa kupigana ngumi za usoni na kuumizana. Mabeki wa kati, Jerome Boateng na Niklas Sule walijaribu kuwagombelezea, lakini tayari walikuwa wameumizana. Hata hivyo, kocha wa Bayern Munich, Niko Kovac hakuwapa adhabu yoyote na waliendelea kufanya mazoezini.

Kinachoelezwa hiyo si mara ya kwanza kwa Lewandowski, ambaye pia anacheza kickboxing kugombana na wachezaji wenzake. Februari 2018 aligombana na beki Mats Hummels mazoezini.

Hata hivyo tukio hilo la Lewandowski na Coman si la kwanza kwa wachezaji wa timu moja kugombana wenyewe kwa wenyewe baada ya kutokea mara kibao tena kwenye viwanja vya mechi za kiushindani.

9. Jamie Carragher vs Alvaro Arbeloa (Liverpool)

Jamie Carragher anapenda mambo mawili, Liverpool na kukaba na wakati mchezaji mwenzake Alvaro Arbeloa alipojaribu kutibua vitu vyake anavyovipenda kwenye mechi moja, ilitosha kumkasirisha na kuwa mbogo. Hiyo ilitokea kwenye mechi ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya West Brom msimu wa 2008/09, ambapo Carragher alimwona mchezaji mwenzake Mhispaniola Arbeloa akifanya uzembe uwanjani na hivyo kuanza kulumbana naye kwa sababu alihisi kwamba ataleta hasara kwenye mambo anayoyapenda.

8. Mario Balotelli vs Aleksandar Kolarov (Man City)

Ni kitu kisichoshangaza kumwona Mario Balotelli kwenye orodha hii kutokana na utukutu wa Mtaliano huyo. Straika huyo wakati mwingine amekuwa na mambo kama ya kitoto na Machi 2012 alionyesha utoto wake wakati alipogombana na mchezaji mwenzake Aleksandar Kolarov kisa kupiga mpira wa adhabu. Kolarov alitaka kupiga na Balotelli alitaka kupiga yeye. Nahodha wa timu, Vincent Kompany alimwondoa Balotelli kumweka pembeni kuepusha ugomvi zaidi. Licha ya kwamba alifunga mabao mawili kwenye mechi hiyo, Balotelli alitoka uwanjani bila ya kumshika yeyote mkono.

7. Emmanuel Adebayor vs Nicklas Bendtner (Arsenal)

Emmanuel Adebayor ni moja ya mastaa waliogombana na wachezaji wenzao ndani ya uwanja na hilo lilitokea alipokuwa Arsenal. Hata hivyo Ade hajahusika kwenye ugomvi wa aina hiyo mara moja, akiwa Manchester City aligombana na Kolo Toure mazoezini. Alikuwa Arsenal aligombana na Nicklas Bendtner. Wawili hao walikuwa hawaelewani na baada ya kukwepana kwa muda mrefu hatimaye walikuja kuonyesha hasira zao za wazi katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Ligi wakati walipochapwa na mahasimu wao Tottenham Hotspur.

6. Ravel Morrison vs Wilfried Zaha (England U-21)

Licha ya kuongoza 5-0 dhidi ya Lithuania katika mchezo wa michuano ya ubingwa wa Ulaya kwa timu za Under-21, makinda wawili wa England, Wilfried Zaha na Ravel Morrison waligombana wenyewe kwa wenyewe ndani ya uwanja, ambapo Zaha alidai Morrison wakati huo aliyekuwa akichezea klabu ya West Ham United alikuwa hampi pasi uwanjani. Hata hivyo mwisho wa mchezo, wawili hao walimaliza bifu lao mbele ya kocha Gareth Southgate licha ya baadaye kuja kudaiwa kwamba mtukutu Morrison bado aliendeleza bifu.

5. Steve McManaman vs Bruce Grobbelaar (Liverpool)

Kipa wa Liverpool, Bruce Grobbelaar alikuwa akifahamika kutokana na ukorofi wake wa ndani ya uwanja na hili lilikuja kuleta madhara makubwa kwenye mechi ya Merseyside derby mwaka 1993. Kipindi hicho, Steve McManaman akiwa bado kinda, alishindwa kuondoa mpira kwenye eneo la hatari na kusababisha Everton kufunga bao, jambo lililomtibua kipa Grobbelaar. Kipa huyo kwa hasira alimfuata Steve na kusema maneno ya shombo usoni kabla ya kupiga mwenyewe. Steve alikaa kimya na hakufanya kitu chochote.

4. Graeme Le Saux vs David Batty (Blackburn Rovers)

Wakiwa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu England, Blackburn Rovers walikwenda kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 1995 na kukumbana na mambo magumu huko, ambapo waliingia uwanjanni kwenye mechi yao ya mwisho ya hatua ya makundi dhidi ya Spartak Moscow wakiwa hawana matumaini ya kufuzu. Jambo hilo liliwavuruga wachezaji David Batty na Graeme Le Saux wakishindwa kuhimili presha zao na kuamua kupigana wenyewe kwa wenyewe baada ya kujikuta wakigongana kwenye kugombea mpira mmoja. Nahodha Tim Sherwood akagombelezea na bahati nzuri hakuna aliyeonyeshwa kadi.

3. Ricardo Fuller vs Andy Griffin (Stoke City)

Alikasirishwa na kitendo cha nahodha wake kushindwa kuzuia wasifungwe na West Ham United, straika wa Stoke City, Ricardo Fuller alimwonyesha Andy Griffin madhara ya kuachia goli kwa kuamua kwenda kumgombeza.

Jambo hilo lilimfannya staa huyo wa Jamaica kuwa na chuki zaidi na kumpiga kibao cha usoni Griffin na matokeo yake akatolewa uwanjani kwa kadi nyekundu.

Hata baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu Fuller bado aliendelea kumtolea lugha chafu Griffin.

2. Jermaine Beckford vs Eoin Doyle (Preston North End)

Ugomvi mwingine ulioibuka baina ya wachezaji wawili wa timu moja pale mastaa wa Preston North End wakati huo, Jermaine Beckford na Eoin Doyle walipoamua kuzipiga wakati timu yao ilipokuwa ikipambana kusaka bao la kusawazisha dhidi ya Sheffield Wednesday. Beckford alichukizwa na mchezaji mwenzake kushinda kumpa pasi na hivyo kumfuata na kwenda kumsukuma kifuani. Doyle hakukubali akarudishia na matokeo yake wote walionyeshwa kadi nyekundu.

1. Kieron Dyer vs Lee Bowyer (Newcastle United)

Hili bado tukio maarufu zaidi lililowahi kutokea kwa wachezaji wa timu moja kupigana wenyewe kwa wenyewe uwanjani. Lilitokea kwenye siku mbaya ya Newcastle United, ambapo tayari walikuwa wameshachapwa 3-0 na hapo wapo 10 uwanjani kwenye mechi yao dhidi ya Aston Villa. Mambo yalikuwa magumu zaidi baada ya Lee Bowyer na Kieron Dyer walipoamua kukabana koo na kuzipiga wenyewe uwanjani, ambapo Lee Bowyer alianza kurusha ngumi na hivyo akaadhibiwa na timu yake, chama cha soka na polisi.

Advertisement