Lema ampa kaka yake hat trick huko Austria

KISA ni uwepo wa kaka yake, nyota wa Kitanzania, Michael Lema ‘Simba’ amepiga mabao matatu ‘hat trick’ kwenye mchezo wa Ligi daraja la tatu Austria ‘Regionalliga’ dhidi ya Völkermarkt akiwa na kikosi B cha Sturm Graz.

Lema alipata ugeni Austria wa kaka yake Erick ambaye alienda kumtembelea na kuwa miongoni mwa watazamaji 450 waliopata nafasi ya kuushuhudia mchezo huo wa Regionalliga kwenye Uwanja wa Lilienberg.

Nyota huyo wa Kitanzania, alisema amejisikia faraja kuwepo kwa kaka yake kwenye mchezo huo na kubainisha ndiyo sababu iliyomfanya kuwa na njaa zaidi ya kufunga ili kutoa zawadi mabao hayo kwa familia yake kwa jumla.

“Kaka yangu amenipongeza kwa kuonyesha kiwango kizuri, nilipanga kufunga ili aone mdogo wake ninavyopambana kutimizia ndoto zangu. Anajua kuwa ninatamani kuwa mchezaji mkubwa Ulaya.

“Nilivyopata moja sikuchoka ukawa mwanzo wa kutafuta lingine na mwishowe nikajikuta nafunga matatu.Ile ni hat trick yangu ya kwanza kwenye mashindano,” alisema Lema ambaye anamudu kucheza nafasi zote za ushambuliaji.

Lema alifunga mabao hayo matatu Ijumaa ya mwisho wa mwezi uliopita dakika ya 17, 42 na 90. Nyota huyo wa Kitanzania ambaye ni mzaliwa wa Itigi mkoani Singida aliisaidia timu yake B kuibuka na ushindi wa mabao 4-1.

Erick kwa upande wake alisema mdogo wake anaweza kufika mbali kama ataendelea kuwa na njaa ya mabao ambayo aliionyesha kwenye mchezo huo ambao alifunga mabao matatu.

“Kikubwa anatakiwa kuendelea kujituma anaweza kuwa mchezaji mkubwa ambaye Tanzania itajivunia kupitia yeye, tukiwa na kina Samatta wengi ni faida kwa taifa letu,” alisema kaka huyo wa Lema.

Lema mwenye miaka 19, amepachika mabao 10 kwenye michezo 10 ya Ligi Daraja la Tatu Austria akiwa na kikosi B cha Sturm Graz.

Mwanzoni mwa msimu wa 2018/19, Lema alipandishwa kikosi cha kwanza ambacho kipo Ligi Kuu Austria lakini kukosa kwake nafasi ya kucheza aliombewa nafasi ya kurejea kikosi cha vijana ili aendelee kupata uzoefu kabla ya kuanza kutumika.