Lango la stars lipo salama vigezo vitaamua nani akae

Muktasari:

  • Maisha yanaenda kasi msimu uliopita wakati Yohana Mkomola anatua Yanga alikuwa kwenye moto wa kuotea mbali na sasa amesahaulika kana kwamba hayupo kutokana na muda mwingi kukaa benchi kwa kukosa nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza.

HEKA heka za nani atafuzu kwenda Cameroon kucheza fainali za Afcon mwaka kesho (2019) zinazidi kupamba moto na tayari baadhi ya timu zimekata tiketi ya michuano hiyo, nyingine zikiwa zinaendelea kupambana kutafuta nafasi.

Kila nchi inatamani kuipata nafasi hii kwa sababu nyingi zikiwa pamoja na zile za kijamii, kiutamaduni, kisiasa na kiuchumi lakini kubwa kuliko yote ni kuweka historia itakayobeba jina la nchi na watu wake kwa kipindi kirefu kupitia mchezo wa soka.

Michuano hii inachezwa kila baada ya miaka miwili, watanzania tumeendelea kuwa watazamaji kwa zaidi ya miaka thelathini na nane (38) tangu tuliposhiriki kwa mara ya kwanza na ya mwisho mwaka 1980 nchini huko Nigeria.

Katika hali ya kawaida lazima tukiri kuwa michuano hii imekuwa migumu kwetu, kwa sababu tumejaribu kusaka nafasi ya kushiriki mara kadhaa bila mafanikio yoyote licha ya juhudi mbalimbali kufanywa na viongozi pamoja na wadau wa soka hapa nchini.

Katika nadharia za kuonyesha kuwa maisha ni mapambano na yana changamoto zake, kuna usemi mmoja mpaka kwenye vitabu vya dini kuwa “ni makosa makubwa sana binadamu kukata tamaa katika maisha”, hususani tunapokuwa tunatafuta mafanikio.

Kwa kuuelewa usemi huu na ukweli wake katika tafsiri pana, wananchi, wadau na mamlaka zenye wajibu na dhamana ya kuilea, kuijenga na kuisimamia timu yetu ya taifa (Taifa Stars) kwa nyakati tofauti, wamekuwa na juhudi za pamoja katika kupanga na kutekeleza mipango ili kuhakikisha nchi inakuwa miongoni mwa mataifa tishio katika soka barani Afrika na ikiwezekana duniani kote lakini bado hatujafika tunapopataka.

Kitaalamu soka ni mchezo unaozungukwa na misingi ya kisayansi katika kuucheza, kuendesha na kuukuza, hivyo taratibu za mchezo zinahitaji kukubaliana na ukweli, kwa hiyo hakuna njia ya mkato itakayokusaidia kupata mafanikio bila kuhusisha taaluma ya saikolojia, falsafa, sosholojia, fizikia, kemia, hisabati, uongozi na utawala unaozingatia sayansi katika mifumo ya kuendesha mambo.

Shirikisho la soka Tanzania (TFF) wamekuwa na kawaida ya kutafuta wataalamu kutoka ndani au nje ya nchi kwa ajili ya kusimamia benchi la ufundi lenye weledi wa kutosha ili kuipa timu yetu mafanikio chanya ambayo ni endelevu.

Orodha ya walimu waliowahi kuitwa na kupewa jukumu la kuinoa Taifa Stars ni ndefu na kila aliyebahatika kupewa kandarasi kuifundisa Stars alijaribu kufanya alichoweza katika kufundishisha na kuwalea wachezaji na kila mmoja atakumbukwa kwa mchango wake katika maendeleo ya soka hapa Tanzania.

Safari hii ni zamu ya mwalimu, Emmanuel Amunike kutoka Nigeria ambaye kwa muda mfupi aliokaa hapa tangu mwezi wa saba mwaka huu ameanza kujipambanua katika baadhi ya mambo ya kiufundi.

Miongoni mwa majukumu makubwa ya msingi ya mwalimu yeyote katika ngazi ya timu ya taifa au hata katika ngazi ya klabu ni kuchagua/kutafuta wachezaji popote pale walipo ili aunde kikosi kitakachompa matokeo ya ushindi.

Inawezekana mwalimu wetu amefanya hivyo pia licha ya kuwa na muda mfupi kwenye benchi la ufundi kama kiongozi, huenda hakupata muda wa kutosha kuizunguka nchi yetu yote ili awe na wigo mkubwa zaidi wa kuviona vipaji lukuki vilivyopo nchini kwetu.

Kwa kuzingatia kwamba muda haukuwa rafiki kabla ya kuendelea na kampeni ya kushiriki fainali za Afcon kwenye mchezo wake wa kwanza dhidi ya Uganda ugenini, nina imani hakuweza kufanya hivyo kama yeye lakini kwa kushirikiana na kurugenzi ya ufundi ndani ya Shirikisho ameweza kuwaita nyota wengi aliowaona wana sifa na vigezo vinavyostahili kuchezea timu ya taifa ya Tanzania.

Kwa mara ya kwanza wapenzi na wadau wa soka hapa nyumbani tumeshuhudia mwalimu akiwaita kikosini Walinda Mlango wanne kwa wakati mmoja na kizuri zaidi wote wamekuwa ni sehemu ya kikosi hata kwenye safari za nje, Uganda na Cape Verde. Walinda mlango hao ni Aishi Manula (Simba), Beno Kakolanya (Yanga), Mohamed Abdulrhaman (JKU), Benedict Tinoko (Mtibwa) na Aron Kalambo (Prisons) aliyeitwa kuchukua nafasi ya Abdulrhaman aliyepata majeraha kambini wakati timu ikiwa inajiandaa na safari ya kwenda Cape Verde.

Kama nilivyotaja hapo awali kwamba mchezo huu unasimamiwa na kuendeshwa kwa misingi ya kitaaluma zaidi, kwa kipengere hiki cha mwalimu kuwaita walinda mlango wengi kwa wakati mmoja.

Kitendo hicho kinatafsiri mtindo wake katika ufundishaji lakini pia kile anachokiamini na kukielewa katika nafasi mbali mbali wakati timu ikiwa inatekeleza majukumu yake, kuanzia mazoezini mpaka kwenye mchezo wa ushindani, kwa kifupi hii ni falsafa yake katika kufundisha na kuandaa timu (Coaching Philosophy and Style).

Tumezoea kuwaona walinda mlango watatu na baadaye wanachujwa na kubaki wawili, lakini safari hii mpaka kwenye mchezo dhidi ya Cape Verde Uwanja wa Taifa, walinda mlango wote wanne walipasha mwili joto na kukaa benchi tayari wakisubiri lolote litakalotokea mwalimu aweze kuamua kumtumia mmojawapo kati yao.

Kama ilivyo kwa asili (nature), kila mtu amepewa karama zake na Mungu, hawa wote ni wachezaji tena wanaoitumikia nafasi moja ya kulinda lango lakini kwa njia mbali mbali ukiwatazama kwa muonekano wa nje hawafanani vivyo hivyo hata kipaji chao hakifanani.

Akili na uwezo wao wa kufikiri na kutenda/kufanya mambo haufanani lakini ni wazuri ndiyo maana wameitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa.

Mara nyingi nguvu na udhaifu wa wachezaji unategemea kila mmoja anavyowatazama kwa kuzingatia yeye anataka kuona nini kinafanyika tena kwa usahihi, kiufundi yapo mambo makubwa matatu ya msingi, uwezo mzuri wa kiakili kulingana nafasi husika, mbinu na ufundi na mwisho utimamu wa mwili.

Walinda Mlango hawa wote ni wanyumbufu, wepesi na wanafanana katika kuzuia mpira ya aina mbali mbali, siyo waoga, na wana weza kuwasiliana vizuri na walinzi.

Kasoro walizonazo ndogo ndogo kila mmoja zinajitokeza kwenye nguvu za kuhimili mikiki mikiki hasa wakati wa mashambulizi ya kustukiza, kufanya maamuzi ya haraka, matumizi ya nguvu za mwili wakati wa kukabiliana na wapinzani.

Sambamba na hayo yote, wanatofautiana kidogo kwenye ubora wa kugawa mipira baada ya kuidaka pamoja na uwezo wa kupiga mipira mbali (goli kiki).

Kimsingi tofauti zao ndogo ndogo katika mbinu na ufundi ndiyo zizomfaya mwalimu amtumie Aishi Manula na kuwa chaguo lake la kwanza kwa sasa na wenzake wakiendelea kusubiri.

Hii ina maana mwalimu anazingatia uwezo wa kila mmoja katika kuifanya kazi yake vizuri zaidi ili kuipa timu matokeo chanya hususani kwa kutofanya makosa ya kizembe ya mara kwa mara yanayoweza kuigharimu timu.