Lampard vs Solskjaer ,arteta kazi anayo

Muktasari:

Man United watakwenda Stamford na kiungo wao huyo wakimtarajia akafanye mambo makubwa baada ya kuonyesha ubora katika mechi yake ya kwanza dhidi ya Wolves kabla ya ligi kuingia kwenye mapumziko.

LONDON, ENGLAND. MAMBO iko Stamford Bridge hapo keshokutwa Jumatatu. Kitapigwa kipute cha maana, Chelsea na Manchester United.

Vita ya kisasi baina ya Frank Lampard na Ole Gunnar Solskjaer. Mechi ya kwanza timu hizo zilipokutana, The Blues ilikubali kichapo cha mabao 4-0 uwanjani Old Trafford. Hiyo Jumatatu mambo ni moto.

Beki wa zamani wa Liverpool, Jamie Carragher amemtisha kiungo mpya wa Man United, Bruno Fernandes kwamba akae akijua kwamba atakutana na kitu kipya kabisa kwenye mechi yake ya pili ya Ligi Kuu England hiyo Jumatatu.

Man United watakwenda Stamford na kiungo wao huyo wakimtarajia akafanye mambo makubwa baada ya kuonyesha ubora katika mechi yake ya kwanza dhidi ya Wolves kabla ya ligi kuingia kwenye mapumziko.

Carragher anaamini Fernandes atakwenda kukutana na wakati mgumu wakati atakapokabiliana na viungo wa Stamford Bridge.

“Siku zote nawafikiria viungo wa Chelsea kwa sababu inao wa nguvu sana kama Jorginho, Kante na Kovacic. Kuna Mason Mount na Ross Barkley, ambao wanaweza kuingia kwenye sehemu hiyo pia ya katikati ya uwanja,” alisema.

Man United wanasubiri kupunguza pengo la pointi katika kuisogelea Chelsea kwenye Top Four.

Man United kwenye nafasi ya nane, wamekusanya pointi 35, pointi sita nyuma ya Chelsea waliopo kwenye Top Four. Wanaamini ushindi utawafanya kupunguza pengo hilo na kubaki pointi tatu kwenye mchakamchaka wao wa kuifukuzia Top Four ili kukamatia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Macho ya wengi yatakuwa kwenye mchezo huo. Mechi nyingine za ligi hiyo usiku wa jana Ijumaa, Wolves walitarajia kukipiga na Leicester City, lakini shughuli itakuwa leo Jumamosi, ambapo Southampton watakuwa na kazi mbele ya Burnley. Mechi hiyo ya St Mary’s itakuwa na upinzani mkali kwa sababu kila timu itapambana kujiondoa kwenye hatari ya kushuka chini kwenye shimo la kushuka daraja. Kipute kingine, Liverpool wataanza ile kampeni yao ya kusaka ushindi kwenye mechi sita ili kubeba taji lao la kwanza la Ligi Kuu England baada kusubiri kwa miaka 30.

Wababe hao wanaonolewa na kocha Jurgen Klopp watakuwa ugenini kwa Norwich City kumkabili Teemu Pukki na wenzake, huku ushindi wowote kwa Liverpool basi utawafanya kuweka pengo la pointi 25 dhidi ya Man City kwenye nafasi ya pili, au pointi 24 kama Leicester City watakuwa wameshinda mechi yao ya usiku wa jana huko Molineux.

Kesho Jumapili zitapigwa mechi mbili, ambapo Aston Villa ya Mbwana Samatta itapambana kujiondoa kwenye nafasi za chini wakati itakapokipiga na Spurs ya Jose Mourinho huko Villa Park. Spurs wenyewe watahitaji kushinda mechi hiyo ili kuikaribia Top Four, ambapo kwa sasa wamepitwa pointi 4 na Chelsea walio kwenye nafasi hiyo.

Arsenal wao watakuwa na kampeni ya kutafuta pointi za kupanda juu wakati itakapowakabili Newcastle United uwanjani Emirates. Arsenal inahitaji ushindi kwa nguvu zote kwenye mechi hiyo ili kuweka sawa kibarua cha Mikel Arteta, ambaye tayari ameanza kujadiliwa kama kweli ni mtu sahihi katika kurudisha makali kwenye kikosi hicho. Jumatatu ndio kitapigwa kipute cha kibabe, The Blues watakapokuwa Stamford Bridge kuwakabili Mashetani Wekundu wa Old Trafford.