Kwa nini Van Dijik asipewe?

Muktasari:

Ni kweli, Cristiano Ronaldo na Lionel Messi pamoja na uhodari wao wote lakini walipewa tuzo ya mwanasoka bora wa dunia mara nyingi kwa sababu ya kufunga. Wana uwezo wa kufunga mabao 50 na zaidi kwa kila msimu.

DAKIKA 450 zimebakia. Ligi Kuu ya England. Sergio Kun Aguero mtoto wa Buenos Aires ana mabao 19. Mohamed Salah, mtoto wa Nagrig pale Misri ana mabao 18. Kwa nini tuzo ya mwanasoka bora wa msimu huu asipewe Virgil van Dijik? Najiuliza.

Mpira wa soka unaendeshwa na wahuni. Wachezaji wahuni, wanaoongoza wahuni, mashabiki wahuni. Kwa miaka mingi sasa wameamua wanaofunga zaidi ndio ambao wanatazamwa zaidi. Mara nyingi mfungaji bora ugeuka kuwa mchezjai bora wa msimu. Imekuwa kitu cha kawaida dunia nzima. Nadhani umuhimu wa mabao umeongezeka kuliko wakati mwingine wowote.

Ni kweli, Cristiano Ronaldo na Lionel Messi pamoja na uhodari wao wote lakini walipewa tuzo ya mwanasoka bora wa dunia mara nyingi kwa sababu ya kufunga. Wana uwezo wa kufunga mabao 50 na zaidi kwa kila msimu.

Mlinzi wa mwisho kutwaa tuzo ya mwanasoka bora wa dunia alikuwa Fabio Cannavaro mwaka 2006. Sijui nini kilitokea kwa washambuliaji. Mlinzi wa mwisho kuchukua tuzo ya mwanasoka bora wa England alikuwa John Terry. Mwaka 2005. Sijui kilitokea nini kwa washambuliaji.

Kwa nini mwaka huu asiwe Virgil van Dijik? Mara chache huwa inatokea kwa mabeki pale washambuliaji wamezubaa. Zimebakia dakika 450 za soka Ligi kuu England na sioni mshambuliaji ambaye atafikisha mabao 30 ya msimu.

Msimu uliopita Mo Salah alifunga mabao 32 na alichaguliwa kuwa mchezaji bora. Msimu huu zimebakia mechi tano ana mabao 18. Mfungaji bora wa kumfikia Salah inabidi apigie Hat trick nne katika mechi tano zilibaki sioni hilo likifanyika.

Ni katika msimu kama huu ndipo anapotafutwa mlinzi mbabe au kiungo maridadi wa kuchukua nafasi hiyo. Ndipo jina la Virgil van Dijik linapojitokea.

Moja kati ya sababu ya washambuliaji kutong’ara katika msimu huu ni kushindwa kutuonyesha mapungufu ya Van Dijik kwa wale washambuliaji ambao sio wa timu yake.

Van Dijik anabaka, anasambaza mipira, mzuri hewani, mzuri chini, zaidi anaonea washambuliaji. Hili ndilo haswa ambalo linanishangaza Ligi kuu England. Wamekwenda wapi kina Didier Drogba, Wayne Rooney, Duncan Ferguson? Hili kidogo linanishangaza.

Kabla ya Van Dijik tulikuwa na walinzi wababe hapo nyuma. Kina Nemanja Vidic, John Terry, Martin Keown na wengineo. Lakini bado kuna wakati walikutana na wababe ambao waliwageuza kuwa asusa tu.

Kwa mfano, unakumbuka jinsi Fernando Torres alivyokuwa anamwonea Nemanja Vidic? Unakumbuka jinsi Didier Drogba alikuwa anawaburuza kina Sol Campbell? Vipi kuhusu Wayne Rooney na kina Vincent Kompany?

Hata hivyo, msimu huu Van Dijik anaonekana kufanya mambo makubwa ya kipekee kuliko wote hao. Sawa, ubora wake unachangia kwa kiasi kikubwa hasa kwa hili umbo lake la kibabe, pia washambuliaji ni wanyonge. Anawanyanyasa. Anawaonea.

Hakuna mshambuliaji aliyewahi kumburuza Van Dijik hadharani. Anafanya kazi zake za msingi pia anajitokeza kufanya kazi za walinzi wake wa pembeni akiwa Andy Robertson na Alexander Arnold. Hapa ndipo unapompa tuzo hii.

Huwa inatokea mara chache na inapotokea ni hapo hapo beki anapopata fursa. Msimu ujao unaweza kuwa tofauti na Van Dijik akawa uchochoro kama walinzi wengine lakini kwa kile alichoonyesha msimu huu huku mshambuliaji bora mpaka sasa akiwa na mabao 19 ni wazi sasa Van Dijik anaweza kupewa.

Awali nilikuwa nawaangalia zaidi washambuliaji ambao ndio pia huwa wanaangaliwa na wahuni wengi tuliojaa katika soka. Lakini kwa hali ilivyo inaonekana wazi labda Sterling anaweza kumsumbua Van Dijik.

Sterling mwenyewe anakuja bila ya mabao. Anakuja kwa sababu ya kiwango zaidi.

Zipo nyakati ambazo kina Vincent Kompany walitisha sana lakini hawakuweza kukuchukua hizo tuzo kwa sababu ya ubabe wa washambuliaji. Kama wangetamba katika msimu huu nadhani nao wangeweza kuondoka na tuzo.

Ni hadithi ile ile ya Messi na Ronaldo. Sisi wahuni wa mpira tumewahi kuwanyima mastaa wengi tuzo hiyo kwa sababu ya kuangalia tu ubabe wao wa mabao. Inakuaje Andres Iniesta hakuwahi kutwaa tuzo ile? Inakuaje Wesley Sneijder hakuwahi kutwaa tuzo ile? Vile Xavi Hernandez?

Bila ya mabao ya Ronaldo na Messi wangechukua. Ni kama ambavyo msimu huu bila ya mabao ya kutosha ya akina Salah na Aguero basi inabidi Van Dijik apewe. NamWona kabisa mfungaji bora akiwa na mabao 23 au 24 msimu huu.

Kama wameshuka kutoka mabao 32 hadi 24 kwanini Van Dijik asichukue tuzo? Wakati Terry akiwa mlinzi wa mwisho kuchukua tuzo hiyo mfungaji bora alikuwa Henry na mabao 25 tu. inaweza kujirudi msimu huu.